1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa marafiki wa Syria

22 Oktoba 2013

Mataifa ya Kiarabu na yale ya Magharibi yamekutana mjini London Jumanne (22.10.2013) kuwashinikiza viongozi wa upinzani wa Syria kuhudhuria mazungumzo ya Geneva mwezi ujao kwa kwenda na kauli moja.

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi marafiki wa Syria katika mkutano wa London. (22.10.2014).
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi marafiki wa Syria katika mkutano wa London. (22.10.2014).Picha: Oli Scarff/AFP/Getty Images

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague amesema mkutano huo ulikuwa na lengo la kuyashawishi makundi ya waasi wa Syria kuwa na msimamo mmoja wakati wa mkutano unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa uliopangwa kufanyika mjini Geneva Uswisi hapo tarehe 23 mwezi wa Novemba.

Hata hivyo akiendelea na ukaidi wake Rais Assad wa Syria amesema yuko tayari kugombania kuchaguliwa tena katika uchaguzi hapo mwaka 2014 hatua ambayo inazidi kulighadhibisha kundi kuu la waasi ambalo lilikuwa linakataa kushiriki mkutano huo wa pili wa Geneva iwapo viongozi wa serikali ya Syria watashiriki.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo amesema lengo ni kuwa na mchakato wa kisiasa kwa kuandaa mkutano wa amani wa Geneva kwa kuishirikisha serikali ya Syria na upinzani ambapo Assad hatakuwa na dhima yoyote katika serikali mpya ya Syria.

Assad hana dhima katika serikali mpya

Amekaririwa akisema njia pekee ya kukomesha mzozo huu na mateso ya raia wasiokuwa na hatia wa Syria ni kwa kupitia kipindi cha mpito cha mchakato wa kisiasa nchini Syria. Madhumuni ya mkutano huu ni kutuma ujumbe wa azma yao na umoja wao kufanikisha hilo. Hague ameongeza kusema kwamba wamekubaliana juu ya hatua mbali mbali muhimu za kuchukuwa ambapo Assad hatakuwa na dhima yoyote ile katika serikali ijayo ya Syria.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague (kulia) na Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry (kushoto)wakiwasili katika mkutano wa marafiki wa Syria huko London. (22.10.2013)Picha: picture-alliance/dpa

Kwa mujibu wa Hague mkutano huo ni kwa ajili ya kuwashajiisha wawakilishi wa upinzani kuwa na msimamo wa pamoja kuionyesha dunia miongoni mwa mataifa ya Kiarabu na Magharibi ambayo yanafahamu na kukubaliana na msimamo wao nchini Syria kwamba wana msimamo mmoja na kwamba wanapaswa kuhudhuria mazungumzo ya Geneva na kuzungumza wakiwa kitu kimoja kama Wasyria na kukomesha umwagaji damu nchini humo.

Mataifa rafiki wa Syria

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry pia amehudhuria mazungumzo hayo pamoja na wenzake kutoka Misri,Ufaransa, Ujerumani,Italia,Jordan,Qatar Saudi Arabia,Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Urusi ambayo ni mshirika muhimu wa Syria ambayo huko nyuma imekuwa ikiipuuza mikutano ya aina hii kwa kusema kuwa haiwakilishi wananchi wote wa Syria haikushiriki mkutano huo.

Baraza la Taifa la Syria ambalo ni chombo muhimu katika Muungano wa Taifa wa Syria tayari lilikuwa limesema kwamba linapinga mkutano wa Geneva na kutishia kujitowa kwenye kundi kuu linalounganisha wapinzani wa Syria iwapo serikali ya Assad itashiriki mkutano huo.

Mustafa Sabbagh (kushoto), Katibu Mkuu wa Baraza la Taifa la Syria na Burhan Ghalioun (kulia), Rais wa zamani wa Baraza la Taifa la Syria.Picha: Reuters

Wwawakilishi wa upinzani wa Syria wanatazamiwa kukutana mapema mwezi wa Novemba kuondowa tafauti zao.

Rais Assad alitowa pigo hapo awali kwa matumaini ya amani kwa kusema katika mahojiano hapo jana kwamba sababu za kufanikisha mkutano huo hazipo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW