1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa masuala ya Diesel wakubaliana

3 Agosti 2017

Wakuu wa makampuni ya uzalishaji wa magari nchini Ujerumani wamekubaliana kutumia kiasi cha Euro Milioni 500 katika kuboresha programu za kompyuta kwenye magari milioni 5.3 yanayotumia dizeli.

Deutschland Dieselgipfel in Berlin | Zetsche, Müller, Wissmann & Krüger
Picha: picture-alliance/dpa/M. Gambarini

Wakuu wa makampuni ya kutengeneza magari nchini Ujerumani wamekubaliana hapo jana katika mkutano wa kilele uliowakutanisha na viongozi wa kisiasa kutumia kiasi cha Euro Milioni 500, sawa na Dola Milioni 592 katika kuboresha programu za kompyuta katika magari milioni 5.3 yanayotumia nishati ya dizeli, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kurejesha imani kwenye sekta hiyo iliyochafuka. 

Wakati makampuni ya kutengeneza magari yalionekana kuepuka shinikizo la kisiasa lililotaka mabadiliko ya gharama kubwa zaidi za vifaa, waziri wa Mazingira Barbara Hendricks alisisitiza kuwa maboresho ya programu yalikuwa ni hatua ya awali kuelekea kuboresha viwango vya uchafuzi wa hewa.

Hendricks alikiri mbele ya waandishi wa habari baada ya mkutano huo kwamba maazimio pekee yaliyofikiwa katika mkutano huo hayatajitosheleza.

Waziri Mkuu wa Jimbo la Kati la Lower Saxony, ambako ndiko makao ya kampuni ya magari ya Volkswagen, Stephan Weil amesema msukumo wa kuboreshwa kwa programu hizo utaendelea.

Watengenezaji hao wa magari waliokutana mjini Berlin, Volkswagen, pamoja na chapa zake za kifahari Audi na Porsche, BMW, Daimer, Ford ya Ujerumani na chapa inayomilikiwa ka kampuni ya Ufaransa, Opel, wamekubalina kuboresha programu hizo kama sehemu ya hatua za mfululizo za kushughulikia mzozo unaovikabili viwanda vinavyotengeneza magari yanayotumia dizeli.

Sekta ya magari imechafuka kutokana na tuhuma zilizofichuliwa kuhusu udanganyifu wa vifaa vya kupima utoaji wa gesi chafuPicha: picture-alliance/dpa/C. Klose

Sekta ya magari lilitikishwa mnamo mwezi Septemba 2015, wakati Volkswagen ilipokiri kufunga vifaa kwenye magari yake ambavyo vinatoa taarifa za uongo za vipimo vya nishati ya dizeli katika uchafuzi wa mazingira kwa zaidi ya magari milioni 11 duniani kote.

Mzozo huo uliongezeka baada ya vyombo vya habari kuripoti kuhusu makampuni matano ya magari, Volkswagen, Audi, Porsche, BMW na Daimler, yalikuwa yameunda genge la siri la wafanyabiashara ambao miongoni mwa mambo mengine hujadiliana kuhusu viwango na namna ya kudhibiti utoaji wa gesi chafu tangu miaka ya 1990.

Utafiti wa maoni uliotolewa na taasisi ya YouGov siku ya jana ulionyesha kuwa ni asilimia 41 tu ya Wajerumani wenye imani ya sekta ya magari, ambayo inaajiri kiasi ya watu 828,000, inayowakilisha asilimia 14 ya nguvu kazi kwenye sekta ya uzalishaji nchini Ujerumani.

Mkutano huo pia uliunda sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa shirikisho la Ujerumani utakaofanyika Septemba 24, huku chama cha Kansela Angela Merkel cha CDU kikikosolewa kwa kuendeleza uhusiano uliopitiliza na watengenezaji wa magari na namna kilivyoshughulikia mzozo wa uchafuzi wa hewa.

Mkutano huo ambao ulihusisha mawaziri wakuu wa majimbo matano ya Ujerumani ambako ndiko yaliko makao makuu ya makampuni ya magari hayo pia ulikubaliana kutoa kiasi cha Euro Milioni 500 kushughulikia matatizo ya uchafuzi wa mazingira ya mijini, na  kuanzisha mfuko wa ruzuku unayolenga kuboresha na kuendeleza mifumo ya usafi kwenye sekta ya usafiri wa mijini.

Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE.

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW