1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

LUXEMBOURG.

Mtullya, Abdu Said7 Oktoba 2008

Mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya wakubaliana kuchukua hatua thabiti kulinda akiba za watu na kuimarisha mfumo wa fedha barani Ulaya.

Waziri wa fedha wa Ufaransa Christine Lagard.Picha: AP

Mawaziri wa fedha wa nchi za Umoja wa Ulaya wamekubaliana kwenye kikao chao cha dharura kilichofanyika Luxembourg leo, juu ya kuyasaidia mabenki makubwa yanayokabiliwa na matatizo katika nchi zao ili kuyaepusha mabenki hayo na mfumo wote wa fedha kufilisika.

Mawaziri hao pia wamekubaliana juu ya kulinda akiba za watu binafsi kwenye mabenki.Akizungumza na wandishi habari baada ya kikao hicho ,waziri wa fedha wa Ufaransa Christine Lagarde amesema nchi za Umoja wa Ulaya zimesimama pamoja , kwa uthabiti wote katika kuukabili mgogoro wa fedha na kwamba zitaratibisha juhudi zao.Baada ya kuongoza kikao cha hicho cha dharura cha mawaziri wa fedha wa nchi zote 27 za Umoja wa Ulaya kwa niaba ya nchi yake ambayo ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja huo, waziri Lagarde ameeleza kuwa nchi zote zimekubaliana kuhakikisha uthabiti na utengemavu katika mfumo wa fedha wa jumuiya yao, na zitachukua kila hatua.

Waziri Lagarde pia amefahamisha kuwa serikali za nchi za Umoja wa Ulaya zitabeba dhamana ya kulinda akiba za watu kwenye mabenki hadi kiasi cha Euro 50,000. Kwa mujibu wa utaratibu uliokuwa unaotumika hadi sasa serikali zilikuwa zinachukua dhamana ya kuhakikisha akiba hizo, hadi kiasi cha Euro 20,000 tu. Kwenye kikao chao cha leo mawaziri wa fedha wa Ulaya pia wamekubaliana kupandisha kiwango cha dhamana.

Mawaziri hao wa fedha wa nchi za Umoja wa Ulaya wamefikia maamuzi hayo ili kurejesha uhakika katika mfumo wa fedha na kuwaondolea wananchi wao, wasiwasi. Na kwa ajili hiyo nchi za Ulaya zimeahidi kudumisha utengemavu katika mfumo wa fedha kwa kutenga fedha zaidi kwa kupitia kwenye mabenki yao makuu na pia zimeahidi kushirikiana na kila benki binafsi.

Wakati huo huo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel leo anatarajiwa kulihutubia bunge juu ya mgogoro wa fedha ulioikumba nchi yake vilevile.