1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua za ulinzi zaimarishwa

15 Aprili 2015

Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa G7 mjini Luebeck,na wito wa Estonia kutaka majeshi ya jumuiya ya kujihami ya NATO yawekwe katika eneo la Baltik miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi magazetini

Mawaziri wa Mambo ya nchi za nje wa G7 katika mkutano wao mjini LuebeckPicha: Reuters/D. Reinhardt

Tunaanzia lakini kaskazini ya Ujerumani,ambako polisi wameenea katika kila pembe ya mji huo wa kale- Luebeck kuzuwia machafuko wakati mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi saba zilizoendelea kiviwanda - G7 ukiendelea kwa siku ya pili hii leo.Gazeti la Flensburger Tagesblatt linasema picha inayojitokeza wakaazi wa Luebeck hawatoisahau milele.Gazeti linaendelea kuandika:"Baada ya machafuko makubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa mbele ya jengo la benki kuu ya Ulaya mjini Frankfurt,idara ya usalama haikuwa na njia nyengine isipokuwa kutuma idadi kubwa kabisa ya polisi kulinda usalama katika eneo la kale kati kati ya mji wa Luebeck.Wakaazi wa Luebeck hawatoisahau milele picha ya kuzingirwa na polisi lango mashuhuri la "Holstentor.".Kwa kuwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry anahitaji hatua za ulinzi sawa na zile za rais Obama,linazuka suala kuhusu gharama na faida ya mkutano wa maandalizi ya mkutano wa kilele wa G7.Hata wataalam wa wizara wangeweza kukutana badala yao na kuandaa taarifa ya mwisho ya mkutano wa kilele.Wakaazi wa Luebeck wanajiliwaza kwa sababu mkutano wa maandalizi wa mawaziri wa fedha wa G7 ungepelekea kuwepo hatua kubwa zaidi za ulinzi.Kishindo kama hicho tayari kinakutikana Dresden kwenye malumbano kati ya makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia na yale ya siasa kali ya mrengo wa kushoto.

Faida za mikutano ya kilele ya G7

Gazeti la kaskazini ya Ujerumani "Kieler Nachrichten" linahisi mikutano kama hii haina budi kuitishwa.

Maandamano ya wapinzani wa G7Picha: picture-alliance/dpa/M. Scholz

"Madai yanayotolewa kila mara kutaka mkutano wa kilele wa G7 ufanyike kwa njia ya simu,ni ya hadaa.Diplomasia haiendeshwi kwa simu.Migogoro mfano wa ule wa Mashariki ya kati au maradhi hatari ya Ebola barani Afrika inahitaji baadhi ya wakati mazungumzo ya ana kwa ana kati ya mataifa yanayoongoza kiuchumi duniani.Na hilo hata wapinzani wa G7 wanapaswa kulitambua .Wahuni wasiochelea kutumia nguvu ndio chanzo cha kutengwa wale wanaoandamana kwa amani."

Nchi za Baltik zinahitaji ulinzi wa NATO

Wasi wasi umeenea katika baadhi ya nchi za kambi ya mashariki ya zamani,zikihofia yasije yakawafika yale yale yaliyotokea Crimea.Kuhusu wasi wasi huo linaandika gazeti la "Badische Zeitung" linalozungumzia kuhusu wito wa Estonia wa kutumwa vikosi vya NATO katika eneo hilo."Tangu Vladimir Putin alipoanzisha vita vya kichini chini dhidi ya Ukraine na kuiteka ardhi ya Crimea,watu katika eneo la Baltik wameingiwa na wasi wasi balaa kama hilo lisije likawakumba.Ndio maana viongozi wa serikali mijini Tallinn,Riga na Vilnius wanapigania tangu muda mrefu sasa vikosi vya jumuiya ya kujihami ya NATO viwekwe katika nchi zao.Kwa hivyo ilikua ikitarajiwa kumuona waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani Ursula von der Leyen,akiwa ziarani hivi sasa nchini Estonia,akizongwa na maombi hayo.Ursula von der Leyen akasema kile kinahostahiki kusemwa:"Kwamba jukumu la kusaidia linazihusu pia nchi za Baltik."Pakitokea mzozo kwa hivyo NATO itabidi iwasaidie pia washirika hao.Hata hivyo wanajeshi wa NATO hawatowekwa milele katika eneo hilo.Kwasababu hakuna anaetaka kuwaona wanajeshi wa NATO wakikabiliana uso kwa macho na wale wa Urusi katika eneo hilo.

Waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani Ursula von der Leyen ziarani mjini VilniusPicha: picture-alliance/dpa/M. Gambarini

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Gakuba Daniel