Mkutano wa mawaziri wa NATo mjini Vilnius
7 Februari 2008Matangazo
Mawaziri wa ulinzi wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO wanakutana mjini Vilnius nchini Lithuania kuanzia leo.Mada kuu katika mkutano huo wa siku mbili inahusu Afghanistan.
Imekua desturi sasa kua kila mkutano muhimu wa jumuia ya kujihami ya magharibi unapokurubia kuitishwa,panazuka mijadala moto moto juu ya namna ya kugawana majukumu magumu yanayosababishwa na opereshini kubwa kabisa ya jumuia hiyo nchini Afghanistan.Wanajeshi 43 elfu wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO wamewekwa nchini humo tangu miaka minane iliyopita.
Marekani inayochangia idadi kubwa ya wanajeshi hao,inawashinikiza washirika wake ndani ya jumuia hiyo ya kujihami ya NATO watume wanajeshi zaidi katika maeneo ya kusini ya Afghanistan.Waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates amewatumia tumia risala tena za maandishi,washirika wao ikiwa ni pamoja na Ujerumani kuwataka watume wanajeshi zaidi na waruhusu wakati huo huo wanajeshi wao wapelekwe pia katika maeneo ya kusini badala ya kusalia pekee katika maeneo tulivu ya kaskazini.
Mwito wake kwa Ujerumani umeshakataliwa na serikali kuu mjini Berlin.
Waziri wa ulinzi wa Marekani anatazamiwa hata hivyo kushadidia hoja zake hii leo mawaziri wa ulinzi wa jumuia ya kujihami ya NATO watakapokutana mjini Vilnius nchini Lithuania.
"Nnahofia jumuia isije ikageuka ya makundi mawili ambapo baadhi ya washirika wako tayari kupigana na kufa ili kulinda usalama wa binaadam na wengine ambao hawako tayari kufanya hivyo".
Afghanistan imewatia mbioni pia mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice na mwenzake wa Uengereza David Miliband.Wote wawili wamewasili kwa ghafla hii leo nchini humo wakitokea London .Walikwenda kwanza katika eneo la kusini la Kandahar-kwenye uwanja wa mapambano kati ya vikosi vya NATO na waasi wa Taliban.Wamepangiwa kuonana na wakuu wa kijeshi wa Nato kabla ya kurejea Kaboul kwa mazungumzo pamoja na rais Hamid Karzai na wanasiasa wengine wa Afghanistan.
Ziara hii ya pamoja ya mawaziri wa mambo ya nchi za njje wa Marekani na Uengereza inatoa picha ya mshikamano ulioko kati ya nchi hizo mbili katika suala la kuwajibika jumuia ya kujihami ya magharibi NATO nchini Afghanistan. Akiwa ziarani mjini London waziri Condoleezza Rice alisema hapo awali:
"Tunataka kuona jumuia ya kujihami inatekeleza jukumu lake kama ilivyo ahidi,yaani kudhamini usalama wa wananchi wa nchini Afghanistan.Ni dhahir kwa hivyo kwamba tunahitaji kugawana majukumu." Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy alidokeza december mwaka jana,huenda nchi yake ikazidisha idadi ya wanajeshi wake nchini Afghanistan ili kuwasaidia polisi na wanajeshi wa Afghanistan.
►
Matangazo