Mkutano wa mazingira Katowice wakaribia kufikia tamati
11 Desemba 2018Lengo ni kufikia muda uliopangwa wa mwishoni mwa mwaka katika kupatikana makubaliano ya utaratibu juu ya vipi kuchukua hatua za kupunguza zaidi hali ya ongezeko la joto duniani.
Mawaziri na wakuu wa nchi kutoka karibu nchi 130 wamekuwa wakiwasili na wataanza kutoa hotuba za ufunguzi jioni ya leo. Wakati huo huo , vikosi vyao vya majadiliano vinafanyakazi kwa faragha kuwezesha kuandika mswada juu ya sheria kwa ajili ya utekelezaji wa makubaliano ya Paris ifikapo jioni leo. Jana waziri mkuu wa zaani wa Ufaransa Ufaransa Laurent Fabius , ambaye aliongoza makubaliano ya Paris mwaka 2015, alisema atashangazwa iwapo hakutapatikana makubaliano kuhusiana na utaratibu utakaofuatwa ifikapo mwishoni mwa wiki lakini kiwango cha hamasa ni suala linalotia shaka.
"Kutokana na ripoti za hivi karibuni za kisayansi ambazo zimepatikana, tarakimu ni mbaya na hatupo katika njia sahihi, kwa hiyo tunapashwa kuwa na dhamira zaidi. hapo ndio majadiliano yatatoa matunda ama la katika dakika za mwisho," amewaambia waandishi habari.
Taifa la kisiwani katika bahari ya Pasifiki la Vanuantu limetoa wito wa kuundwa kwa mfuko mpya wa "hasara na uharibifu" kuhakikisdha malipo kutoka mataifa tajiri, na yenye viwanda , kwenda katika mataifa yale yaliyoathirika zaidi na maafa ya mazingira.
Ushirika utasaidia kupunguza ujoto
Joto la wastani duniani linaelekea kupindukia lengo kuu lililowekwa katika makubaliano ya Paris mwaka 2015 la kupunguza ujoto duniani, uchunguzi umeonesha leo Jumanne. Mwakilishi maalum wa China katika mkutano wa Katowice Xie Zhenhua ushirikiano wa mataifa utasaidia kupunguza ujoto duniani.
"Ushirikiano wa dunia katika nishati utasaidia kuondokana na matumizi ya nishati ya mafuta na mkaa na kuanza kutumia nishati salama, na hii itakuwa hatua muhimu katika kutatua matatizo ya utoaji wa gesi za kaboni na kuweza kufikia lengo la kudhibiti ujoto kufikia nyuzi joto 2 na hata 1.5."
Lakini ongezeko hilo ifikapo mwishoni mwa karne hii huenda ikawa chini ya kiwango cha juu mno kuliko inavyotarajiwa kutokana na juhudi maalum zinazofanywa na baadhi ya mataifa kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, imesema ripoti ya hatua za kufuatilia mabadiliko ya tabia nchi , iliyoandikwa na kundi la makundi huru matatu yanayofanya utafiti katika bara la Ulaya.
Makubaliano ya Paris yanalenga kuzuwia ongezeko la ujoto kufikia chini ya nyuzi joto mbili katika kipimo cha Celsius juu ya enzi za kabla ya viwanda.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Josephat Charo