1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mazingira wa UN wafunguliwa rasmi Glasgow

31 Oktoba 2021

Viongozi wa dunia watalazimika kuweka wazi juhudi zao za kupunguza joto duniani baada ya miaka 6 tangu yalipofikiwa makubaliano ya Paris

UK Glasgow | Protest vor COP26
Picha: Andrew Milligan/PA Wire/picture alliance

Mkutano wa kilele wa mazingira wa Umoja wa mataifa umefunguliwa rasmi huko Glogow nchini Scotland, Uingereza ukitarajiwa kuendelea kwa wiki mbili za mazungumzo ya kina ya kidiplomasia ambayo yanazishirikisha kiasi nchi 200 za dunia.

Mazungumzo hayo yataangazia kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto ya pamoja ya ongezeko la joto duniani.

Katika ufunguzi leo Jumapili maafisa walianza kwa kuyaangalia masuala muhimu yakujadiliwa kabla ya duru itakayowakutanisha viongozi wa juu kutoka nchi mbalimbali za dunia.

Viongozi wa dunia wataweka wazi mipango yao ya jitihada za kukabiliana na gesi chafu zinazochafua mazingira pamoja na hatua za kupambana na madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Mengi ya masuala yanayojadiliwa kwenye mkutano huo wa COP26 utakaokwenda hadi Novemba 12 yamekuwa kwenye agenda kwa miongo sasa ikiwemo suala la namna ambayo nchi tajiri zinavyoweza kuzisaidia nchi masikini kukabiliana na uchafuzi wa mazingira na kuwa na uwezo wa kuishi katika mazingira ya ongezeko la joto kali.

Kwa hakika mwenendo wa kujikongoja wa kuchukuliwa hatua umewakasirisha sana wanaharakati wengi wanaoendesha kampeini ya kutetea mazingira ambao wanatarajiwa kuanzisha maandamano makubwa wakati wa mkutano huu ya kupiga kelele hatua zichukuliwe.

Mwenyekiti anayeondoka wa mazungumzo haya kutoka Chile Carolina Schmidt ameyafungua mazungumzo ya Glosgow kwa kuwataka maafisa kukaa kimya kwa dakika moja kwa ajili ya kuwapa heshima watu waliopoteza maisha kutokana na janga la Covid-19 tangu mkutano wa mwisho wa mazingira uliofanyika mwishoni mwa mwaka 2019.

Picha: COP26 Coalition

Viongozi wa dunia watakusanyika kesho Jumatatu kushiriki mkutano huo.

Mkutano huo utalenga kuwaona wajumbe kutoka nchi takriban 200 wakijaribu kuyatafutia ufumbuzi masuala yaliyoachwa pembeni tangu yalipofikiwa makubaliano ya mazingira ya Paris mnamo mwaka 2015 na kusaka njia ya kuimarisha juhudi za kuzuia viwango vya joto visipindukie nyuzi joto 1.5 za kipimo cha Celsius.

Ingawa wanasayansi wanasema nafasi ya kufikia lengo hilo muda wake unayoyoma. Jumatatu mwanamfalme Charles atawakaribisha viongozi wa dunia mjini Glasgow.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW