Mkutano wa NAM: Mursi ataka waasi wa Syria waungwe mkono
30 Agosti 2012Imebidi Iran, mwenyeji wa mkutano huo, kuonesha kiwango cha juu cha uvumilivu, pale wawili kati ya viongozi muhimu kutoa kauli isizozitegemea kwenye kikao cha ufunguzi wa mkutano huo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, alitumia hotuba yake kuushambulia vikali msimamo wa Iran kuelekea taifa la Israel na kuiita kuwa haukubaliki.
"Kudai kwamba mwanachama mwengine wa Umoja wa Mataifa, Israel, haina haki ya kuwepo au kuizungumzia kwa maneno ya kibaguzi sio tu kwamba si sahihi, bali pia kunahujumu misingi ambayo sote tumeapa kuilinda." Alisema Ban Ki-moon.
Mara kadhaa, Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran amekuwa akisema kwamba kile kinachoitwa "mauaji ya maangamizi dhidi ya Mayahudi barani Ulaya" ni hadithi ya kubuni tu, huku pia akiielezea Israel kama "saratani ya ubongo" isiyopastahiki kuwepo.
Mursi ataka waasi Syria waungwe mkono
Kwa upande wake, Rais Mohammed Mursi wa Misri ametumia hotuba yake ya ufunguzi kuunga mkono upinzani nchini Syria, na kuutaka ulimwengu kuwasaidia wale aliowaita "wapiganiaji uhuru na haki dhidi ya utawala wa kikandamizaji" wa Rais Bashar al-Assad.
"Dola ya watu wa Misri iliyotokana na mapinduzi ya umma ni kigezo kwa Wimbi la Mageuzi ya Arabuni yaliyoanzia Tunisia.... Na sasa mapinduzi yako Syria dhidi ya utawala wa kidhalimu." Alisema Mursi.
Msimamo huu unatafautiana sana na wa Syria na Iran ambao wanawaita waasi nchini Syria kuwa ni "magaidi" wanaotimiza mpango wa Marekani na majirani wa Syria.
Iran ni mshirika mkubwa wa utawala wa Assad, na kauli hii ya Rais Mursi inachukuliwa kama kibao cha uso kwa mwenyeji wake, Rais Ahmadinejad.
Ujumbe wa Syria watoka nje
Ujumbe wa Syria kwenye mkutano huo ulitoka nje kulalamikia kauli hiyo ya Rais Mursi, na baadaye Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Walid al-Muallim, aliielezea kauli hiyo kama "inayochochea umwagaji damu na uingiliaji wa mambo ya ndani ya Syria."
Hata hivyo, mkutano huo ulitoa fursa kwa Rais Ahmadinejad kukutana na mgeni wake, Rais Morsi, katika mazungumzo ya faragha.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hussein Amir Abdullahian, amekiambia kituo cha habari ya al-Alam kwamba viongozi hao wawili walijadiliana mgogoro wa Syria na mahusiano ya nchi zao.
"Walisisitiza haja ya kutatua mgogoro wa Syria kwa diplomasia na kuzuia uingiliaji kati wa mataifa ya nje. Na pia walijadiliana njia za kuimarisha mahusiano kati ya Misri na Iran." Alisema Abdullahian.
Rais Mursi amehudhuria mkutano huo wa mataifa yasiyofungamana na upande wowote, pamoja na mengine, kukabidhi uwenyekiti wa jumuiya hiyo kwa Iran. Uongozi wa jumuiya hiyo huenda kwa mzunguuko na sasa ni zamu ya Iran.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman