1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Mkutano wa nchi za kiislamu waanza Pakistan

22 Machi 2022

Maazimio kiasi 100 ya kisiasa kupitishwa na mawaziri wa mambo ya nje wa jumuiya ya OIC mjini Islamabad,miongoni mwao ni kuhusu msaada kwa Afghanistan na kuwaunga mkono Palestina

Pakistan Afghanistan OIC Konferenz
Picha: Rahmat Gul/AP/picture alliance

Mawaziri wa mambo ya nje wa  jumuiya ya ushirikiano wa nchi za  kiislamu wameanza mkutano wao unaofanyika nchini Pakistan hii leo, ukiwa na malengo kadhaa muhimu ikiwemo kuidhinisha msaada wa kifedha kwa ajili ya Afghanistan na kuwaunga mkono wapalestina na jimbo la Kashmir.

Mkutano wa mjini Islamabad wa jumuiya ya nchi za kiislamu OIC unafanyika chini ya kauli mbiu inayosema ushirikiano kwa ajili ya Umoja,haki na maendeleo na kiongozi wa Pakistan Imran Khan atatowa hotuba muhimu ambayo bila shaka itagusia azimio la wiki iliyopita la Umoja wa Maataifa ambayo itakuwa ya msisimko mkubwa kuwahi kutowa tangu alipochaguliwa waziri mkuu Agosti mwaka 2018.

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran KhanPicha: Rahmat Gul/AP Photo/picture alliance

Mkutano wa OIC una agenda yenye malengo ambayo yanajumuisha kuidhinisha maazimio 100 ikiwa ni pamoja na suala la kuisadia kifedha Afghanistan,kuwaunga mkono Wapalestina na jimbo la Kashmir. Mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi za kiislamu pia unahudhuriwa na waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi licha ya kwamba Beijing inakosolewa kwa namna ambavyo inaishughulikia jamii  ya waislamu katika mkoa wa Xinjiang. Kwa upande wmingine pamoja na kwamba maafisa wamempongeza waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan kwa hotuba aliyoitowa mbele ya hadhara ya Umoja wa mataifa wiki iliyopita na  kuufanya Umoja huo kutambuwa rasmi chuki dhidi ya waislamu kuwa kitisho cha kidunia,mwanasiasa huyo aliyewahi zamani kuwa mcheza kriketi anakabiliwa na kura ya kutokuwa na imani nao katika bunge la nchi yake.

Aidha mkutano huu wa leo unafanyika katika wiki yenye shughuli nyingi katika medani ya siasa nchini humo ambapo kesho Jumatano nchi hiyo pia inaadhimisha siku ya Pakistan,ambapo litafanyika gwaride la kijeshi na maonyesho ya ndege za wanaanga.

Ikumbukwe Imran Khan aliingia madarakani katika wakati nchi hiyo ikishuhudia mvutano kwenye uchaguzi wa kambi kuu mbili zilizokuwa zimezoeleka kuhodhi siasa za taifa hilo lakini hivi sasa kiongozi huyo inaonyesha amepoteza uungwaji mkono pengine ukiwemo pia ule  wa jeshi.   

Kaimu Waziri wa Mambo ya nje wa Afghanistan Amir Khan MuttaqiPicha: Rahmat Gul/AP Photo/picture alliance

Khan amewatolea mwito mamilioni ya wafuasi wake kukusanyika wiki ijayo katika mji mkuu Islamabad kuwashinikiza wabunge chungunzima wa bunge la taifa ambao wanatajwa kufikiria uwezekano wa kumpigia kura ya kutokuwa na imani nae.

Lakini kwa upande mwingine viongozi wa vyama viwili vikuu vya upinzani nao pia wamewatolea mwito wafuasi wao kukusanyika hali ambayo imewafanya maafisa nchini Pakistan kuitangaza wiki hii kuwa ya mapumziko ili kujaribu kuepusha mgogoro kuzuka na hasa katika kipindi cha mkutano huu wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za kiislamu. 

Wachambuzi wanasema inavyoonesha serikali na vyama vya upinzani wako kwenye mkondo wa kuingia kwenye mvutano na hawaelekei kutaka kutafuta suluhisho la matatizo yaliyoko kisiasa na badala yake wanajaribu kuoneshana nguvu kupitia wafuasi wao mitaani.

Kimsingi muswaada wa kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu Khan umepangwa kuwasilishwa rasmi ijumaa huku mchakato wa kura ukitazamiwa kufanyika wiki ijayo.

Na mkutano wa leo wa OIC unaangaliwa kama kikao cha kupiga domo ambacho kitapitisha msururu wa maazimio ya kisiaasa na kubwa miongoni mwa maazimio hayo ni lile linalohusu kuisadia Afghanistan japokuwa hakuna uwezekano wa kikao hicho kuitambua rasmi serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na Taliban.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW