Mkutano wa OPEC Vienna
27 Novemba 2014Nchi 12 wanachama wa shirika la Opec wanakutana baadae mjini Vienna nchini Uswisi katika mkutano unaotajwa kuwa mgumu na muhimu zaidi huku wanachama hao wakitolewa mwito wa kuchukua hatua za kueleweka baada ya bei za mafuta kushuka kwa asilimia 30 tangu mwezi Juni.
Mataifa ya Ghuba yanayotoa mafuta kwa wingi yakiongozwa na Saudi Arabia yanatarajiwa kuzihimiza nchi nyingine wanachama kutochukua hatua ya kupunguza uzalishaji licha ya baadhi ya wanachama kusikika wakitoa miito ya kupunguza uzalishaji wa mafuta ghafi kama hatua ya kuimarisha bei za bidhaa hiyo muhimu duniani iliyokwisha teremka vibaya.
Mjumbe mmoja kutoka nchi za Ghuba aliyezungumza na shirika la habari la Uingereza Reuters amesema shirika hilo la Opec halielekea kuchukua hatua za kupunguza uzalisha katika mkutano wa leo ingawa kuna baadhi ya wajumbe wanaoashiria kwamba matokeo ya mazungumzo ya leo hayawezi kutabirika.Ikiwa wanachama hao wa OPEC watakubaliana dhidi ya hatua ya kupunguza uzalishaji wa bidhaa hiyo na kuongeza kiwango kilichoko hivi sasa hatua hiyo itamaanisha kuanza kwa vita vya bei ya mafuta ambavyo nchi kama Saudi Arabia na wazalishaji wengine wa eneo la Ghuba itavimudu kutokana na akiba zao kubwa zinazoingiza fedha za kigeni.
Wanachama wengine kama Venezuela au Iran zitakabiliwa na hali ngumu zaidi ikiwa hilo litafanyika.Waziri wa mafuta wa Iran Bijan Zangeneh akizungumzia suala hilo amesema baadhi ya wanachama wa Opec wanaamini kwamba huu ndio wakati wanaohitajika kutetea masoko yao.wakati wataalamu katika soko la bidhaa hiyo wakiamini kwamba kwa sasa kiwango kilichoko kimepindukia na mwakani kitapindukia zaidi.
Inatajwa kwamba kupindukia huko kwa kiwango cha uzalishaji mafuta ndiko kulikopelekea kwa kiasi kikubwa kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo tangu mwezi Juni na hasa kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya mafuta yasiosafishwa nchini Marekani pamoja na ukuaji wa taratibu wa uchumi China na barani Ulaya.
Ikiwa upande mmoja utachukua uamuzi wa kupunguza kiwango cha uzalishaji wa mafuta basi hatua hiyo itakuwa na athari kubwa kwa shirika hilo la OPEC linalotegemewa kwa thuluthi tatu ya mafuta ya dunia. Lakini hatua hiyo itakuwa pigo kwa soko la mafuta ghafi yanayozalishwa na nchi za Amerika ya Kaskazini. Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi lakini wanahisi mkutano wa Vienna unaofuatiliwa kwa karibu utaamua kubakia na uzalishaji wa mapipa millioni 30 kwa siku kama ilivyo sasa ingawa vile vile upo uwezekano wa kufikia hatua tofauti na hiyo.
Mwandishi Saumu Mwasimba
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman