1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Paris waahidi "Makubaliano Mapya" kwa Afrika

19 Mei 2021

Viongozi wakuu waliohudhuria mkutano wa kilele mjini Paris kwa ajili ya Afrika wamekubaliana jana kuhusu mpango wa kulisaidia bara hilo kukabiliana na athari za janga la virusi vya corona.

Frankreich Gipfel Abdel Fattah el-Sissi und Emmanuel Macron
Mwenyeji wa mkutano wa kilele wa Paris, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akimkaribisha rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sissi kwenye mkutano huo, Mei 17, 2021.Picha: Christophe Ena/AP Photo/picture alliance

Mwenyeji wa mkutano huo, rais wa Ufransa Emmanuel Macron, amesema wamechukua hatua ya kwanza katika kile walichokubaliana kukiita "makubaliano mapya na Afrika".

Macron alisema mkutano huo wa kilele ulikubaliana kufanya kazi kuyashawishi mataifa tajiri kutenga tena kiasi cha dola bilioni 100 katika fuko maalumu la shirika la fedha la kimataifa IMF kwa ajili ya mataifa ya Afrika kufikia Oktoba.

Mkurugenzi Mtendaji wa IMF Kristalina Georgieva, alikuwa amethibitisha kuwa shirika hilo litatoa dola bilioni 33 kwa ajili ya bara la Afrika mwaka huu katika mpango maalumu unaosaidia kufadhili manunuzi ya nje.

Mwenyeji wa mkutano wa kilele wa Paris, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiwa na Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla HamdokPicha: Ludovic Marin/AFP

Mkutano wa kilele wa Paris unanuwia kuzidisha kiwango hicho mara tatu. "Hatuwezi kumudu kuiacha nyuma Afrika," lilisema tangazo la mwisho la mkutano huo.

Soma pia: Africa itatue matatizo yake yenyewe

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Felix Tshisekedi, ambaye ndiye mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, aliutaja mkutano huo kama fursa kubwa kwa Afrika, na kuongeza kuwa janga la virusi vya Corona limeziacha chumi za bara hilo zikiwa hohe hahe kwa sababu walilaazimika kutumia njia zote walizokuwa nazo kupambana na janga hilo.

Na vipi kuhusu chanjo za Covid-19?

Macron amesema washiriki wa mkutano huo pia walikubaliana kuwa bara la Afrika linapaswa kuwa na uwezo wa uzalishaji mkubwa wa chanjo kwa ajili ya wakaazi wake kupitia uhamishaji wa teknolojia na kuondoa vikwazo vya hati miliki.

Soma pia: Viongozi wa Marekani na Afrika wageukia biashara

Suala hili likatiliwa mkazo pia na rais Tshisekedi. "Ni kweli kwamba kuna wasiwasi fulani, nitakiri kama mwafrika na rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo," alisema rais Tshisekedi.

Rais wa Angola Joao Lourenco na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Afrika Moussa Faki.Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

"Watu wetu hawajahamasishwa vya kutosha kuhusu chanjo. Wasiwasi kwa maoni yangu unatokana na ukweli kwamba chanjo inatoka nje. Ndiyo maana ni muhimu kulenga kutengeneza chanjo barani Afrika. Nadhani itakuwa na athari muhimu kwa mtazamo wa watu."

Macron ameweka shabaha ya kuchanja asilimia 40 ya watu barani Afrika, kufikia mwishoni mwa mwaka 2021. Rais wa Senegal Macky Sall, alibainisha kuwa utoaji chanjo haukuwa wajibu wa pamoja kwa dunia nzima, na kukumbusha kuwa iwapo chanjo hazitawasilishwa kila mahala, virusi zaidi vinavyojibadili vitaendelea kusambaa.

Soma pia: Kansela Merkel akutana na viongozi 12 wa Afrika mjini Berlin

Afrika Kusini, pamoja na India, zilikuwa zimependekeza uondoaji wa muda wa hataza za chanjo za corona kwa shirika la biashara duniani, WTO. mkutano wa Paris ulihudhiriwa na zaidi ya wakuu 20 wa mataifa ya Afrika, maafisa wandamizi wa Umoja wa Ulaya na shirika la fedha duniani IMF.

Chanzo: Mashirika/DW