1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran: Mlango Bahari wa Hormuz sasa upo wazi

Amina Abubakar afp,reuters,dpa
17 Aprili 2026

Viongozi wa Ufaransa na Uingereza pamoja na viongozi wa Mataifa mengine ya Ulaya wamekusanyika mjini Paris kujadili namna ya kuufungua mlango bahari wa Hormuz, huku Iran na Marekani zikisema tayari njia hiyo iko wazi.

Mlango wa Hormus
Mkutano wa Paris wafanyika huku Mlango Bahari wa Hormruz ukifunguliwaPicha: Altaf Qadri/AP Photo/picture alliance

Mkutano wa Paris ni sehemu ya mataifa hayo kujaribu kupunguza athari ya mgogoro ambao hawakuuanzisha wala kuungana nao, ulioutikisa kwa kiwango kikubwa uchumi wa dunia.  Bei ya mafuta ilipanda maradufu kote duniani baada ya vita hivyo kuanza Februari 28, baada ya Iran kuufunga Mlango Bahari huo ambao asilimia 20 ya mafuta ya dunia hupita.

Kabla ya mkutano wa Paris kuanza, Rais Emmanuel Macron alisema Marekani haikualikwa katika mpango wa juhudi za kuufungua mlango wa Hormuz kwaajili ya uhuru wa safari za meli, akisema mpango huo wa usalama kwa meli zinazopitia eneo hilo ni wa ulinzi na utafanyika wakati hali ya kiusalama itakaporuhusu.

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz na waziri Mkuu wa italia Giorgia Meloni, walikuwepo katika mkutano huo. Viongozi wengine ni Waziri Mkuu wa Australia na Canada pamoja na Korea Kusini na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenski, wote hao walijiunga kupitia njia ya vidio.

Kansela wa Ujerumani Fredrich Merz, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Waziri Mkuu wa Uingereza Kier Starmer na Waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni.Picha: Simon Dawson/Avalon.red/IMAGO

Lakini wakati wawakilishi wa takriban mataifa 50, mashirika ya kimataifa na viongozi wa zaidi ya mataifa 30 wakijiunga na mkutano huo wa Paris hii leo, Rais wa Marekani Donald Trump na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Abbas Araghchi, walitangaza kuwa njia hiyo iko wazi kwa meli zote za biashara.  Araghchi alisema mlango huo utabakia wazi kabisa kwa siku 10 za usitishaji vita kati ya Iran na Marekani.

Bado Marekani itaendelea kuzingira bandari ya Iran

licha ya hayo Trump alisema Meli za Marekani zinazozingira meli za Iran, pamoja na Bandari za Jamhuri hiyo ya kiislamu zitaendelea kufanya hivyo, hadi pale patakapokuwa na makubaliano ya asilimia 100 kati yake na taifa hilo.

Wakati uo huo rais Donald Trump aliandika katika mtandao wake wa Truth Social kwamba, analipinga pendekezo kutoka kwa Jumuiya ya kujihami ya NATO kutaka kusaidia kuufungua mlango bahari wa Hormuz, baada ya Iran kusema mlango huo upo wazi. Trump aliiambia NATO kukaa kando kabisa.

Rais wa Marekani Donald Trump Picha: Mehmet Eser/SOPA Images/ZUMA/picture alliance

Kiongozi huyo wa Marekani alisema,  haoni mantiki ya pendekezo la NATO wakati tayari suala la Hormuz limekamilika na Iran imeshasema kwamba njia hiyo iko wazi. Amesema hataki usaidizi wa NATO akisisitiza kuwa Jumuiya hiyo haikuwepo wakati Marekani ilipoihitaji.

Haya yote yanajiri wakati Israel na wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebabon,  wakikubaliana kusitisha mapigano kwa siku 10 na kuondoa kizuizi kimoja kuelekea kupata muafaka katika mzozo wa Iran.

Haijawa wazi iwapo makubaliano yoyote yatafikiwa kati ya Marekani na Iran kabla ya muda wa mwisho wa usitishwaji vita kwa wiki mbli kati ya mahasimu hao wawili, kumalizika wiki ijayo. Lakini ya hatua kusitishwa vita kati ya Israel na wanamgambo wa Hezbollah wa Lebabon, inaweza kuwa ishara kwamba hatua kadhaa zimepigwa kuelekea lengo hilo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW