1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Poland na Marekani wasusiwa kidiplomasia

13 Februari 2019

Mkutano wa kimataifa juu ya Mashariki ya Kati ulioandaliwa na Poland na Marekani umefunguliwa  huku kukiweko hali ya mashaka kuhusu malengo ya mkutano huo,yakijitokeza masuli juu ya kitakachotokana na mkutano.

Polen, Warschau: Mike Pompeo auf Staatsbesuch
Picha: picture-alliance/M. Wlodarczyk

Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence tayari ameshawasili Poland atakakoshiriki mkutano huo wa kimataifa akiwa pia yuko kwenye ziara ya siku nne barani Ulaya ambapo pia ataitembelea kambi ya maangamizi ya Auschwitz iliyokuwa ikitumiwa na utawala wa Kinazi. Kesho alhamisi atashiriki kwenye mkutano huo wa Mashariki ya kati kabla ya kuelekea kwenye mkutano wa usalama utakaofanyika mjini Munich Ujerumani siku ya Ijumaa.

Mkutano wa Poland awali ulipendekezwa na utawala wa rais Donald Trump kuwa kikao kitakachojikita juu ya Iran lakini waandaaji mkutano huo wakaamua kutanua ajenda zitakazojadiliwa na kujumuisha pia mgogoro wa Israel na Plaestina sambamba na mapambano dhidi ya kundi linalojiita dola la kiislamu,Syria na mgogoro wa Yemen.

Hata hivyo agenda zilizotolewa kuhusu mkutano huo hazioneshi kwa namna yoyote ikiwa zitachukuliwa hatua thabiti ambazo ni zaidi ya kuundwa makundi tu ya kufuatilia hali ilivyo na juu ya hilo nchi takriban 60 zinazoshiriki mkutano huu zitawakilishwa na viongozi wa ngazi za chini serikalini.

Umoja wa Ulaya haujatuma mjumbe 

Picha: picture-alliance/Xinhua News Agency/Li Muzi

Wakati waziri mkuu Benjamin Netanyahu na makamu wa rais wa Marekani Mike Pence wakihudhuria mkutano huu sambamba na waziri wa mambo ya nje Mike Pompeo na wenzake kutoka nchi mbali mbali za kiarabu,Ufaransa na Ujerumani zimeamua hazitotuma maafisa wa ngazi ya uwaziri huku pia mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini akijiweka kando.

Urusi na China hazishiriki mkutano huo na Wapalestina ambao wametowa mwito wa kikao hicho kususiwa pia hawashiriki wakati Iran kwa upande mwingine ikiulaani na kuukosoa mkutano huo kwa kuuita ni kikao cha sarakasi.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif anasema mkutano huo wa siku mbili umeshakufa kabla haujaanza. 

Picha: picture-alliance/AP/R. Drew

Lakini wakati huohuo wakili wa rais Trump aliyekuwa pia wakati mmoja Meya wa jiji la NewYork Rudy Giuliani leo ameshiriki maandamano yaliyoandaliwa na baraza la kitaifa linaloipinga Iran ambalo pia linajulika kama Mujahedeen-e.Khalq au MEK ambalo linajumuisha wairan wanaoishi uhamishoni,wakitowa mwito wa mabadiliko ya utawala nchini Iran.

"Hatupaswi kufanya shughuli zozote na nchi inayounga mkono ugaidi.Hatupaswi kuiruhusu nchi inayosafirisha ugaidi kuwa seehemu  ya jamii ya nchi zenye uhalali.zinapaswa kutengwa.Hivyo ndivyo tulivyokuwa tukizifanya nchi kama hizo. Hii ni nchi yenye uongozi uliojaa damu nyingi  mikononi mwake kuliko nchi nyingine yoyote duniani. Ni nchi iliyosababisha kwa kiwango kikubwa ukosefu wa uthabiti mashariki ya kati.Tazama kinachoendelea Lebanon,angalia kilichopo Syria.Tazama fikra zao juu ya Israel''

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anategemewa kuitumia fursa ya mkutano wa Poland kunadi hadharani jinsi uhusiano wa nchi yake ulivyoimarika na Mataifa  kadhaa ya Ghuba ya Arabubuni.  Kwa mujibu wa agenda makamu wa rais Mike Pence atahutubia mkutano huo kuhusu masuala mbali mbali ya kanda ya Mashariki ya kati wkaati Pompeo atakuwa na jukumu la kuzungumzia kuhusu mpango wa Marekani juu ya Syria kufuatia uamuzi wa rais Trump wa kuondowa wanajeshi wake. Jared Kushner ambaye ni mshauri mkuu wa Trumo na mkwewe atazungumzia mpango ambao haujajulikana bado kuhusu amani ya Mashariki ya Kati.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Iddi Ssessanga