1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Republican: Melania Trump ampigia debe mmewe

Daniel Gakuba
26 Agosti 2020

Katika siku ya pili ya mkutano mkuu wa chama cha Republican nchini Marekani, mke wa Rais Donald Trump, Melania, amevutia hisia kwa kuyamulika madhira ya COVID-19 na kuhimiza utengamano wa watu wenye rangi tofauti.

Washington Weißes Haus Rede Melania Trump vor Parteitag der Republikaner
Melania Trump akiuhutubia mkutano mkuu wa chama cha RepublicanPicha: Reuters/K. Lamarque

Hotuba zilizotolewa na wajumbe wa chama cha Republican mnamo siku hiyo  ya pili ya mkutano mkuu, zimejikita hasa katika kuonyesha sura nzuri ya chama hicho chini ya utawala wa Donald Trump.

Aliyeng'ara zaidi miongoni mwa wajumbe hao ni Melania Trump, mke wa rais Trump ambaye kwa kawaida hapendi kujionyesha katika vyombo vya habari na mitandao. Hotuba yake ilijaa hisia kuhusu masuala ya kijamii, ambayo yalipuuzwa kabisa katika siku ya kwanza ya mkutano huo ulioanza Jumatatu.

COVID-19 imesambaratisha maisha ya wengi

Alizungumzia kadhia ya janga la virusi vya korona, na tofauti na mume wake na pia maafisa wengine wa Trump wanaolizungumzia janga hilo kama tatizo ambalo halipo tena, Melania alisema anatambua fika kuwa tangu mwezi Machi, janga hilo limeyasambaratisha maisha ya Wamarekani wengi, na kusema kutoka moyoni anawapa pole wote waliowapoteza wapendwa wao.

Mkutano Mkuu wa chama cha Republican katika mazingira ya COVID-19Picha: AFP/C. Carlson

Bi Melania pia alilimulika tatizo la ubaguzi wa rangi uliokita mizizi katika jamii ya Kimarekani, huku akiwarai watu wa nchi hiyo kuyazingatia hayo huku wakitazama mbele.

Soma zaidi

''Ni ukweli mchungu kwamba hatuna fahari na sehemu ya historia yetu, lakini nawahimiza watu kuangalia mbele, huku wakijifunza kutokana na yaliyopita'', alisema Melania na kuongeza kuwa Wamarekani wanapaswa kukumbuka kuwa sote tuko jamii moja yenye watu wa asili tofauti, iwe ya rangi au dini.

''Mchanganyiko huo ndio unalifanya taifa letu kuwa lenye nguvu, lakini bado kila mmoja anayo mengi ya kujifunza kutoka kwa mwingine.'' Alishauri Bi Melania Trump.

Pompeo azusha utata wa kimaadili

Mike Pompeo, waziri wa mambo ya nje wa MarekaniPicha: Reuters/Republican National Convention

Hotuba nyingine iliyozungumziwa sana ni ile ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo, iliyorikodiwa akiwa mjini Jerusalem, Israel. Si kawaida kwa waziri wa mambo ya nje, ambaye anachukuliwa kama mtumishi wa umma kuliko mwanasiasa, kuhutubia mkutano kama huu.

Pompeo amechukuwa tahadhari akiepuka kumkosoa mpinzani wa Trump katika uchaguzi ujao, Joe Biden, wala chama chake cha Democratic, badala yake amemwagia sifa Rais Trump na sera zake, iwe kuhusu Mashariki ya Kati, iwe juu ya namna alivyozishupalia Iran, China na Urusi, na kuliangusha Kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.

Kwa hayo yote, Pompeo amedai kuwa utawala wa rais Donald Trump umeimarisha usalama wa Marekani, na Wamarekani wote.

Maudhui muhimu kutoka mkutano wa jana ni ujumbe wa Bi Melania Trump wa kutaka kuwatoa watu hofu kuhusu hulka ya mume wake, akisema, ''Ukweli ndio kitu wanachokihitaji raia wote kutoka kwa rais wao, na ikiwa unaniamini au huniamini, utakubaliana nami kuwa utakijua anachokifikiria Trump.''

 

ap, rtre