1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Mkutano wa Roma hauna maana yoyote."

Maja Dreyer27 Julai 2006

Vita vya Mashariki ya Kati vinabakia kuwa suala kuu ambalo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejihusisha nalo. Leo hii maoni yao yanahusu mkutano uliofanyika mjini Roma pamoja na vifo vya wafanyakazi wanne wa Umoja wa Mataifa.

Tunaanza na matokeo ya mkutano wa mjini Roma uliojaribu kutafuta suluhisho la mzozo huu wa Mashariki ya Kati. Gazeti la “Landeszeitung” la mjini Lüneburg linatoa hukumu kali likiandika:
“Mkutano wa Roma hauna maana yoyote. Nchi zenye mamlaka makubwa duniani zilitoa mwito kuweka chini silaha na kupelekwa kwa jeshi la Umoja wa Mataifa. Lakini jinsi mwito huo usivyofaa ilionekana wazi siku hiyo hiyo kutokana na kuuwawa kwa wanajeshi wanne wa Umoja wa Mataifa. Hata ikiwa mabomu yaliyoshambulia makao ya jeshi la Umoja wa Mataifa hayakupangwa, bado yanaonyesha kutokuwepo kwa suluhu. Operesheni ya amani inafaa tu ikiwa pande zote mbili zinataka amani.”

Gazeti la “Hamburger Abendblatt” linaeleza uelewano kwa msimamo wa Israel. Tunasoma:
“Ni kitu kinachokasirisha kwamba Israel bado inalazimishwa kupigania haki yao ya kuwa taifa. Hata hivyo, mwito wa kuweka chini silaha hautakuwa na matokeo. Je, kuna mtu yeyote anayeamini kundi la Hisbollah litaacha kupigana baada ya kupata heshima mpya katika nchi za Kiarabu? Hapana.”

Mhariri wa “Kieler Nachrichten” lakini anauliza:
“Lini tunaweza kuichukulia Israel kama mwanachama wa jumuija ya kimataifa ambayo ina haki sawa kama mataifa mengine yote, lakini vile vile ina wajibu sawa. Kwa nini wajumbe wa mkutano wa Roma hawakuuliza ikiwa mashambulizi makali ya Israel katika eneo la Lebanon ni dhidi ya sheria ya kimataifa?”

Kuhusu vifo vya wanajeshi wanne wa Umoja wa Ulaya waliouawa na mabomu ya Israel, gazeti la “Märkische Allgemeine” lina hofu ifuatayo:
“Tukio hilo linaharibu sana sifa ya Israel. Vipi sasa tuamini kwamba mashambulizi mjini Beirut yanawaathiri tu wapiganaji wa Hisbollah na siyo raia wa kawaida ikiwa kosa kama hilo la kuwaua wanajeshi wa Umoja wa Ulaya linaweza kutokea?”

Na mwishowe ni gazeti la “Tageszeitung” la mjini Berlin lenye maoni haya:
“Bila ya kujua matokeo ya uchunguzi juu ya tukio hili, ikiwa lilikuwa na makusudi au la: bila shaka kuuawa kwa wanajeshi hawa kutazitia wasi wasi nchi zote zitakazoombwa kushiriki kwenye operesheni mpya ya kijeshi ya Umoja wa Mataifa kwa eneo hilo la mpakani. Na huenda Israel inapendelea hilo.”

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW