1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa SADC wamalizika bila mafanikio

19 Agosti 2011

Viongozi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC jana wamemalizika kikao chao cha siku huko Angola, bila ya kutoa taarifa ya kupiga hatua katika kushughulikia matatizo ya Zimbabwe na Madagascar

Rais wa Angola na mwenyekiti mpya wa SADC Jose Eduardo dos SantosPicha: picture-alliance / dpa

Mikwao ya kisiasa katika nchi mbili mwanachama wa jumuiya hiyo, imekuwa ikigubika ajenda za mikutanao ya SADC katika miaka ya hivi karibuni.

Katika taarifa yao ya pamoja kuhutimisha mkutano huo wa siku mbili, viongozi hao wa SADC,wametaka kutekelezwa kwa wito uliyotolewa katika kikao cha mwezi June cha jumuiya hiyo kilichotaka kuwepo kwa juhudi zaidi za upatanishi kutatua mizozo ya kisiasa katika nchi hizo mbili Zimbabwe na Madagascar.

Kikao hicho kilitilia mkazo uamuzi uliyofikiwa hapo June wa kutaka kufanyika haraka mabadiliko nchini Zimbabwe, lakini hata hivyo wakuu hao hawakutoa mpango wowote wa kutatua mkwamo uliyopo kati ya Rais Robert Mugabe na Waziri wake Mkuu Morgan Tsvangirai kuhusiana na kufanyika kwa uchaguzi mpya nchini Zimbabwe.

Mahasimu hao wawili wa kisiasa waligawana madaraka na kuunda serikali ya umoja chini ya upatanishi wa SADC ili kuumaliza mkwamo wa kisiasa uliyosababishwa na matokeo ya uchaguzi mkuu wa urais mwaka 2008.

Makubaliano hayo yalisaidia angalau kwa kiasi fulani kuunasua uchumi wa nchi hiyo, lakini hata hivyo viongozi hao wamebaki katika mvutano mkubwa wa jinsi ya kutekeleza kufanyika kwa mageuzi halikadhalika tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi.

Viongozi wa SADC katika taarifa yao hiyo ya pamoja jana usiku wamezitaka pande hizo mbili huko Zimbabwe kutekeleza ahadi zao za kufanya mabadiliko waliyokubaliana ili kukamilisha mpango mzima katika kutatua masuala muhimu yaliyokwama.

Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo ya SADC Tomaz Salomao alisema kuwa muundo wa utaratibu wa uchaguzi mpya huko Zimbabwe unakaribia kukamilika, na kwamba pande mbili hasimu zinakaribia kukubaliana juu ya muundo huo.

Ama kuhusiana na mkwamo wa kisiasa huko Madagascar, viongozi hao walielezea kutokuwa na matumaini ya kutekelezwa kwa mpango wa uliyopitishwa wa kufanyika kwa uchaguzi mpya, baada ya aliyekuwa rais Marck Ravalomanana kupinduliwa na meya wa zamani wa jiji la Antananarivo Andy Rajoelina.

Rais wa Angola Jose Eduardo dos Santos, ambaye ni mwenyekiti mpya wa jumuiya hiyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa juhudi za wapatanishi wa jumuiya hiyo katika mzozo wa Madagascar zimekwamishwa.

Ravalomanana amekataa kutia saini mpango huo uliyochini ya upatanishi wa SADC ambao unaelezea kuwa Rajoelina ataendelea kuwa rais wa serikali ya mpito na kumruhusu bwana Ravalomanana kurejea kutoka uhamishoni nchini Afrika Kusini, pale hali ya usalama itakapomridhisha.

Wakati huo huo Mweyekiti huyo mpya wa SADC Rais dos Santos ameitaka NATO kusitisha mashambulio yake dhidi ya Libya akisema harakati hizo za kijeshi zinazuia juhudi za mazungumzo katika kuutanzua mzozo wa nchi hiyo iliyoko kaskazini mwa Afrika.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP

Mhariri:Othman Miraji

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW