Mkutano wa Scholz na Biden, kipi kitarajiwe?
9 Februari 2024Scholz hakutani na Biden akiwa mikono mitupu, kwani siku chache zilizopita, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ziliamua kuisaidia Ukraine na jumla ya euro bilioni 50 mpaka mwaka 2027.
Scholz awali aliupigia chapuo msaada huo, akizingatia pia hali ya kisiasa nchini Marekani.
Akiwa amejawa na ghadhabu, Rais Biden alisema "Kila kitu kinaashiria muswada huu huenda hata usipigiwe kura katika baraza la seneti. Kwa nini? Kwa sababu moja rahisi: Donald Trump. Kwa sababu Donald Trump anadhani ni jambo baya kisiasa kwake."
Soma zaidi: Scholz kuzungumza na Biden juu ya vita vya Ukraine
Ukraine inategemea msaada kutoka kwa Marekani. Saa zinasonga kila wiki, kila mwezi unaopita bila msaada mpya. Hii inamnufaisha Rais wa Urusi Vladimr Putin.
Scholz anataka kusaidia kuutafutia ufumbuzi mkwamo huu mjini Washington kwa kutumia "zawadi ya mgeni" ya euro bilioni 50 kwa Ukraine.
Tija ni ndogo
Hata hivyo, Henning Holf wa Baraza la Mahusiano ya Nchi za Nje anaamini hii haitakuwa na tija yoyote.
"Wabunge wa chama cha Republican wanaonekana hawako tayari kuusaidia utawala wa Biden kwa sababu za uchaguzi. Sasa inabainika zaidi kana kwamba Marekani itajitoa kama mfadhili wa Ukraine." Alisema mtaalamu huyo kwenye mazungumzo yake na DW.
Soma zaidi: Urusi kutozivamia Poland, Latvia
Mshikamano na Ukraine unasambaratika na kwa kuwa Marekani ndio mtoaji muhumi wa silaha kwa Ukraine, hii itakuwa hali mbaya kabisa.
Katika hali kama hii, Rais wa Volodymyr Zelensky Ukraine angependa Ujerumani ichukue jukumu la uongozi na Scholz tayari amewatahadharisha Wajerumani wenzake kwamba Ujerumani huenda ikalazimika kuingilia kati kujaza pengo la Marekani.
Zaidi ya euro bilioni saba tayari zimetengwa katika bajeti ya serikali ya shirikisho kwa ajili ya msaada wa silaha wa Ujerumani mwaka huu.
Ujerumani haina uwezo wa kujaza pengo
Kama Marekani kweli itawacha kuipa msaada Ukraine, bajeti ya Ujerumani itakabiliwa na shinikizo la mizigo zaidi.
Hata hivyo, Scholz akiwa amesimama kama mpatanishi, Ujerumani haiwezi kujaza pengo la dola lenye nguvu kubwa kijeshi kama Marekani.
Msaada kwa ajili ya Ukraine pia unakabiliwa na shinikizo nchini Ujerumani kwenyewe.
Soma zaidi: Scholz: Ninataraji kuwa Bunge la Marekani litaafikiana kuhusu msaada kwa Ukraine
Chaguzi za Ulaya zitafanyika mwezi Juni na kufuatiwa na chaguzi kadhaa za majimbo. Vyama viwili, chama cha mrengo wa kulia cha Alternative for Germany (AfD) na chama kipya cha Sahra Wagenknecht Alliance vinaukosoa msaada kwa Ukraine na vinataka makubaliano na Urusi.
Ukraine haiwezi kujiunga na NATO
Scholz na Biden wanaonekana kukubaliana kwamba mualiko wa Ukraine kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO kwa sasa haupo kwenye ajenda.
Jumuiya hiyo inaweza kuialika Ukraine kwenye mkutano wake wa kilele utakaofanyika mjini Washington msimu wa kiangazi mwaka huu.
Scholz hataki kukutana na Trump wakati wa ziara yake ya Washington.
Je muhula wa pili wa Trump madarakani utakuwa na maana gani kwa mahusiano baina ya Ujerumani na Marekani iwapo atashinda?
Soma zaidi: Maseneta wa Marekani wachapisha rasimu ya msaada wa ziada wa usalama
Henning Hoff anaamini kwamba serikali ya Ujerumani sasa imefanikiwa kufutilia mbali malalamiko ya awali ya Trump kuhusu Ujerumani.
"Kwamba inatumia fedha kidogo kwa ajili ya ulinzi - angalau mwaka huu imevuka juu ya kiwango cha asilimia mbili kilichowekwa na NATO. Kwamba inaitegemea gesi ya Urusi, hilo sasa halipo tena. Kwamba uwiano wa biashara unaipendelea Ujerumani na Ulaya - hilo nalo limebadilika. Biashara ya nje ya Ujerumani kwa sasa kwa namna fulani inadhoofika." Alisema mtaalamu huyo.
Kujiondoa kwa Marekani kutoka NATO kama Trump alivyokuwa akipendekeza mara kwa mara, sasa hakuna uwezekano wa kutokea.
Hii ni kwa sababu Trump atahitaji wingi wa theluthi mbili katika bunge la Marekani, kiunzi ambacho ni kirefu kukivuka.