1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Shirika la Biashara la Dunia, WTO

Lillian Urio27 Julai 2005

Wanachama 148 wa Shirika la Biashara la Duniani, WTO, wameanza majadiliano leo, yatakaoendelea kwa siku tatu, juu ya jinsi ya kuendelea na mazungumzo ya masuala ya biashara za kimataifa, yanaojulikana kama mazungumzo ya Doha.

Mkutano mkuu wa shirika hilo unategemewa kufanyika Hong Kong miezi mitano ijayo na bado kuna baadhi ya wanachama hawaelewani katika mada mbalimbali na wanachama hawa wangependa kuona sheria mbalimbali za biashara za kimataifa zinalegezwa ifikapo mwaka 2006.

Mkutano huu wa siku tatu ulipangwa ili kuangalia ni nini kimefanyika katika takriban miaka minne ya kujadiliana na kuangalia ni yapi wanaweza kufanikisha katika mkutano wa utakaofanyika Hong Kong.

Baadhi ya maafisa wa ngazi ya juu wanaotegemewa kushiriki katika mkutano huu ni pamoja na kiongozi wa masuala ya biashara wa Umoja wa Ulaya, Peter Mandelson na waziri wa biashara wa India, Kamal Nath.

Wachambuzi wa masuala ya biashara wanasema itawabidi washiriki wafanye kazi kwa bidii katika miezi ijayo kama wanataka kuwa na mafanikio lakini hadi sasa hivi, hali inaoynesha kwamba wanaweza kutimiza malengo yao kabla ya mkutano wa Hong Kong.

Wanadiplomasia wanasema masuala muhimu ya kujadiliwa ni pamoja na ushuru wa bidhaa za kilimo na ruzuku za kusafirisha bidhaa hizo nje ya nchi, hasa katika nchi tajiri, vizuizi vya ushuru vya bidhaa za viwandani na mipango maalum kwa nchi maskini.

Lengo kuu la mazungumzo ya Doha, yalioanza nchini Qatar mwaka 2001, ni kuwa na makubaliano ya kupunguza vizingiti katika biashara na kutumia biashara kuzisaidia nchi zinazoendelea.

Wanachama wa WTO wanajaribu kuzuia yasitokee kama yale ya mkutano wao wa 2003 wa mjini Cancun huko Mexico, yaliopelekea mkutano huo kushindwa.

Matatizo makubwa yaliyotokea kwenye mkutano huo ni juu ya masuala ya biashara za kilimo, suala muhimu kwa nchi maskini na masuala ya biashara katika sekta ya huduma, jambo lililokuwa muhimu kwa nchi tajiri.

Mwaka jana wanachama walipiga hatua za kumaliza matatizo yao kwa kukubaliana kuzingatia masuala ya kilimo yatakayowawezesha kuendela na majadiliano.

Lakini hadi hadi sasa wameshindwa kufika mbali katika majadiliano yao. Pia waliamua ifikapo mwezi Julai mwaka 2005 kama, watakuwa na wameandika jaribio la kwanza la nyaraka ya juu ya makubaliano ya kibiashara.

Inasemekana kwamba wanachama wamejiwekea malengo ambayo ni magumu kuyatekeleza. Lakini wanadiplomasia wa masuala ya kibiashara wamesema wana matumaini, wakiongeza kwamba kuna hatua ndogo zimefikiwa kwenye majadiliano.

Kumekuwa na ushirikiano mzuri katika kujadili masuala ya biashara za bidhaa za viwanda. Hata katika suala la kilimo, sasa hivi wameweza kukubaliana matatizo makubwa ya mazungumzo hayo ni juu ya masuala gani. Pia mapendekezo ambayo yana maelezo zaidi kuliko yale ya wakati uliopita yameshawasilishwa.

Kiongozi wa WTO, Supachai Panitchpakdi, anamaliza muda wake wa utawala na wiki hii ndio mara yake ya mwisho ya kujaribu kuendeleza mazungmzo ya Doha.

Bwana Panitchpakdi, kutoka Thailand anamaliza kipindi chake cha uongozi tarehe 31, mwezi Agosti na atamkabidhi Pascal Lamy, ambaye anatoka Ufaransa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW