1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa shirika la fedha la kimataifa mjini Istanbul

Oumilkher Hamidou5 Oktoba 2009

Jinsi bara la Afrika linavyojikwamua kutoka mgogoro wa kiuchumi unaoikaba dunia

Mwenyekiti wa shirika la fedha la kimataifa Dominique Strauss-KahnPicha: picture alliance / dpa

Mgogoro jumla wa kiuchumi umeliaathiri bara la Afrika sawa na sehemu iliyosalia ya dunia.Lakini shirika la fedha la kimataifa IMF linaamini kwamba safari hii mgogoro huu utakua wa muda mfupi tuu na hautaacha madhara makubwa katika eneo la kusini mwa jangwa la sahara,kinyume na ilivyoshuhudiwa katika majanga yaliyopita miaka ya nyuma.

Hakuna nchi yoyote ya bara la Afrika ambayo haikuathirika na mgogoro wa kiuchumi.Kishindo kikubwa zaidi kimepiga katika zile nchi ambazo uchumi wake unategemea nishati kutoka nje na sekta ya utalii.Zaidi ya hayo nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara zimeshuhudia vitega uchumi vya kibinafsi kutoka nje,sawa na fedha zinazopelekwa nyumbani na waafrika wenyewe wanaoishi na kufanya kazi nchi za nje,vikipingua vibaya sana katika kipindi hichi cha mgogoro wa kiuchumi.Matokeo yake yanaonekana katika tarakimu za kiuchumi za shirika la fedha la kimataifa kuhusu eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara,zilizochapishwa mjini Istanbul.Tarakimu hizo zinaonyesha katika kipindi cha mwaka huu ukuaji wa kiuchumi katika eneo hilo utafikia asili mia moja tuu nukta moja.Hilo ni pengo kubwa kabisa watu wakitilia maanani viwango vya ukuaji wa kiuchumi vya kati ya asili mia 5.5 hadi asili mia 7 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Hata hivyo mkuu wa zoni ya Afrika katika shirika la fedha la kimataifa IMF,Antoinette Monsio Sayeh anajiwekea matumaini mema anasema:

"Sio habari zote ni za kuvunja moyo.Tunahisi maamuzi yanayopitishwa na serikali ni ya maana na yatasaidia kuepusha madhara ya kiuchumi kwa nchi kadhaa za Afrika.Sera nyingi za busara za kutoa mikopo midogo midogo zilizokua zikitumika katika nchi nyingi kabla ya mgogoro kuripuka zimezipatia serikali nafuu ya kodi na kudhibiti matumizi licha ya mapato haba."

Shirika la fedha la kimataifa na benki kuu ya dunia barani AfrikaPicha: AP Graphics/DW

Kwa mujibu wa hesabu za shirika la fedha la kimataifa,watu wanaweza kutegemea ukuaji wa kiuchumi wa asili mia nne kwa mwaka 2010 na asili mia 5 kwa mwaka 2011.Ni vyema watu kuangalia maendeleo ya kiuchumi namna yalivyokua miaka ya nyuma, anahisi mkurugenzi wa zoni ya Afrika katika shirika la fedha la kimataifa IMF bibi Antoinette Monsio Sayeh.Kwa maoni yake zamani bara la Afrika lilikua likijikwamua kidogo kidogo baada ya mgogoro wa kiuchumi na lilikua pia dhaifu,likilinganishwa na sehemu iliyosalia ya dunia.Hivi sasa bara la Afrika linajumuika kikamilifu katika mfumo jumla wa kiuchumi wa dunia na ndio maana linaweza kufaidika zaidi na kuchipuka hali jumla ya kiuchumi ulimwenguni.Zaidi ya hayo anahisi bibi Antoinette Monsio Sayeh,serikali nyingi zimejifunza kutokana na makosa ya zamani.

Ili kuweza kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi shirika la fedha la kimataifa limezidisha kiwango cha mikopo.Katika mwaka 2009, shirika la IMF limetenga kitita cha dala bilioni tatu kama mikopo kwa nchi za Afrika kusini mwa jangwa la sahara-kiwango ambacho ni cha juu kikilinganishwa na dala bilioni moja za kimarekani kwa mwaka 2008, au dala milioni 200 kwa mwaka 2007 .

Mwandishi Kohlmann Thomas(DW Wirtschaft)/Hamidou Oummilkhheir

Mhariri:Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW