1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa siku mbili kuhusu Somalia

15 Februari 2012

Serikali ya mpito na Somalia na mashirika kadhaa ya huduma za jamii wanakutana kuzungumzia jinsi ya kujumuishwa koo za nchi hiyo katika serikali mpya huku wakinamama wakidai wabebeshwe jukumu kubwa zaidi .

Ramani ya Somalia

Serikali ya Somalia,serikali za majimbo,mashirika ya jamii na wafuasi wa kundi la kiislam la Ahlu Sunna Wal Jamaa watakutana kuanzia february 15 na kwa muda wa siku mbili huko Garowe katika jimbo la Puntland kuzungumzia muundo wa bunge jipya katika wakati ambapo muda wa serikali ya mpito unamalizika Agosti mwaka huu.

Katika mahojiano ya aina yake pamoja na shirika la habari la IPS,waziri anaeshughulikia maendeleo ya wakinamama na jinsi ya kuitunza familia Dr. Mariam Aweis Jama na mkurugenzi wa masuala ya wakinamama katika kasri la rais,Malyun Sheikh Haidar wamesema wakati umewadia kwa wakinamama wa Somalia kukabidhiwa nafasi muhimu katika ,uongozi wa nchi hiyo.Dr.Maryam Aweis Jama amesema wakinamama wa Somalia wananyimwa nafasi ya uongozi.Amewalaumu wanaume wa Somalia kwa kutowaheshimu wanawake na kuwazuwia kukamata nafasi muhimu zaidi ya kisiasa.

"Nnavyokumbuka mie,katika historia ya nchi hii,mwanamke amekuwa daima akichaguliwa kushughulikia wizara ya wakinamama tu.Lakini wakati umepita sasa ,tunataka tuwakilishwe sawa bin sawa katika baraza jipya la mawaziri."Amesema mkurugenzi wa masuala ya wakinamama katika kasri la rais,Malyun Sheikh Haidar.

Wakinamama wa Somalia wadai madaraka makubwa zaidiPicha: DW

Wote wawili,Jama na Haidar wamesema wanataka kuona wakinamama zaidi wakikabidhiwa wizara tofauti na nyadhifa tofauti za juu nchini humo.

Haidar amesema ni aibu kuona kwamba hakuna hata kiongozi mmoja wa kike katika serikali za majimbo katika nchi hiyo yenye majimbo 18 na mikoa karibu 100.

"Asili mia 70 ya wakaazi wa Somalia ni wanawake na ndio maana dini ya kislam inamruhusu mwanamme aowe hadi wake wanne-kwa hivyo haiwezekani kudharau nafasi ya wakinamama ambao ndio walio wengi."

Jama anasema kulingana na kifungu nambari 29 cha muongozo wa kipindi cha mpito cha Somalia,ulioandaliwa wakati wa mkutano wa suluhu ya taifa uliofanyika Kenya mwaka 2004,wanawake wanabidi wakalie asili mia 12 ya viti vya bunge la mpito.Anahisi kwa hivyo wanadhulumiwa na hawapatiwi nafasi za kutosha katika serikali ya sasa.

44 tu kati ya wabunge 550 wa Somlia ni wanawake.Tume ya haki za binaadam ndio taasisi pekee kati ya 27 za bunge,inayoongozwa na mwanamke.

Wanamgambo wa itikadi kali ya kiislam-Al ShababPicha: AP

Wakinamama wanakabiliana na upinzani mkubwa wa wenzao wa jinsia ya kiume.Wengi hawakubali wanawake wakamate nyadhifa za juu serikalini kwasababu za kidini na kimila.

Sheikh Farah Yusuf,mmojawapo wa maimam katika msikiti Al Huda mjini Mogadischu anafika hadi ya kusema kwamba "uwezo wa kuamua wa mwanamke ni dhaifu kuweza kuiongoza nchi-na kuongeza, nnanukuu" wameruhusiwa kuhudumia familia zao tu.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/IPS

Mhariri: Abdul-Rahman