1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Mkutano wa wakuu wa majeshi wa ECOWAS unaendelea Ghana

17 Agosti 2023

Mkutano wa siku mbili wa wakuu wa Majeshi wa nchi za jumuiya ya kiuchumi ya kanda ya Magharibi mwa Afrika, ECOWAS unaendelea nchini Ghana.

Mkutano wa wakuu wa majeshi wa ECOWAS unaofanyika Accra, Ghana
Mkutano wa wakuu wa majeshi wa ECOWAS unaofanyika Accra, GhanaPicha: Chinedu Asadu/AP Photo/picture alliance

Afisa mmoja mwandamizi amewaambia wakuu hao wa majeshi kwamba nchi za ECOWAS ziko tayari kuingia kijeshi Niger ikiwa juhudi za kuwashawishi watawala wa kijeshi kuondoka madarakani zitashindwa.

Wakuu wa majeshi wa nchi za jumuiya ya ECOWAS wanajadiliana kuhusu namna ya kitakavyokuwa kikosi cha dharura cha kuingia nchini Niger.

Mkutano huo unafanyika katika makao makuu ya jeshi la Ghana mjini Accra.

Waziri wa ulinzi wa Ghana Dominic Nitiwul, akizungumzia kinachoendelea amesema wakuu hao wa majeshi wataandaa mpango kuhakikisha kikosi cha dharura kiko tayari, "Mtaweka mpango wa kuhakikisha kikosi kiko tayari na demokrasia itarudishwa Niger. Nitatumia neno hili, ikiwa walinzi wa rais nchini Guinea na Niger wamewashikilia mateka marais wao, hakuna yeyote na narudia tena, hakuna yeyote katika kanda ya Afrika Magharibi atakayekuwa salama.''

Wanajeshi nchini Niger walimuondowa kwa nguvu rais Mohamed Bazoum Julai 26 na wamekataa kuisikiliza miito iliyotolewa na Umoja wa Mataifa, ECOWAS na nchi za Magharibi ya kuwataka wamrudishe madarakani kiongozi huyo.

ECOWAS kuingilia kati kijeshi Niger

Maandamano ya wafuasi wanaomuunga mkono rais Mohamed Bazoum mjini Paris, UfaransaPicha: Sophie Garcia/AP Photo/picture alliance

Hatua hii ndiyo iliyowachochea wakuu wa nchi za jumuiya ya kiuchumi ya magharibi mwa Afrika ECOWAS kuamrisha kuundwa kikosi cha dharura kitakachokwenda kumsaidia Rais Mohammed Bazoum.

Kamishna wa ECOWAS anayehusika na masuala ya kisiasa amani na usalama Balozi Abdel-Fatau Musah amesisitiza kwamba kikosi hicho lazima kitaingia Niger juhudi za kiplomasia zikishindikana na mkutano wa Accra ndio kithibitsho.

''Mtu yeyote asitilie shaka kwamba ikiwa njia zote zitashindikana vikosi vya nchi za Afrika Magharibi vya kijeshi na kiraia viko tayari kuitikia mwito wa kuchukua majukumu.''

Amewaambia wakuu wa kijeshi katika mkutano wa Accra kwamba kwa namna yoyote utawala wa kikatiba lazima utarudishwa nchini Niger akitaja hatua zilizowahi kuchukuliwa huko nyuma na jumuiya hiyo ya ECOWAS kutatua migogoro nchini Gambia, Liberia na kwengineko kama mifano ya utayarifu wa jumuiya hiyo.

Jenerali Mohamed Toumba wa jeshi la NigerPicha: Balima Boureima/AA/picture alliance

Amewatuhumu wanajeshi wa Niger kwamba wanacheza mchezo wa paka na panya na ECOWAS kwa kukataa kukutana na wajumbe wake, huku wakitafuta njia ya kuhalalisha mapinduzi yao.

Kwa upande mwingine wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imeutaka Umoja wa Ulaya kuwawekea vikwazo watawala hao wa kijeshi wa Niger.

Ujerumani pia imesema inaunga mkono juhudi zinazochukuliwa na ECOWAS kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW