Mkutano wa Syria wataka kuimarisha amani
4 Aprili 2018Taarifa hiyo ya pamoja ya viongozi hao Recep Tayyip Erdogan , Vladimir Putin na Hassan Rouhani iliwekwa katika tovuti ya rais wa Iran baada ya mkutano wao wa kilele uliofanyika mjini Ankara nchini Uturuki.
Viongozi hao walifanya mkutano na kila mmoja wao kwa nyakati tofauti kabla ya kuanza kwa mkutano wa pande tatu, ambao uliiweka kando Marekani , nchi nyingine ya kigeni yenye majeshi yake nchini Syria.
Mataifa hayo matatu yanasukuma kile kinachojulikana kama mchakato wa Astana , ambao una lengo la kuweka "maeneo ya kutuliza vita" nchini Syria. Licha ya hayo, mataifa yote matatu yanabakia kuwa wahusika wakubwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Rais wa Iran Hassan Rouhani ameilaumu Marekani kwa kuliunga mkono kundi la wanamgambo linalojiita Dola la Kiislamu nchini Syria na kutoa wito kwa nchi zote kuheshimu uhuru wa mshirika wake mkubwa katika mataifa ya kiarabu katika mashariki ya kati , imesema televisheni ya Iran.
Baadhi ya nchi ikiwa ni pamoja na Marekani , wanaunga mkono makundi ya kigaidi kama Dola la Kiislamu nchini Syria, ambalo linalinda maslahi ya nchi hizo, Iran ikiamini mzozo wa Syria hauna suluhisho la kijeshi na kuulinda uhuru wa Syria kuwa ni jambo muhimu kwa Tehran," Rouhani aliwaambia waandishi habari mjini Ankara.
Mipaka ya Syria iheshimiwe
Nae rais wa Uturuki Tayyip Erdogan amesema kwamba uhuru wa mipaka ya Syria unategemea kujiweka mbali na makundi yote ya kigaidi , akimaanisha Marekani kuliunga mkono kundi la wanamgambo wa Kikurdi nchini Syria ambalo Uturuki inaliona kuwa ni adui.
Erdogan amesema kwamba matumaini ya kupata mafanikio nchini Syria yanaongezeka. Na kusema kwamba Uturuki na Urusi zitafanyakazi kwa pamoja kujenga hospitali katika eneo la Tel Abyad nchini Syria kuwatibu wale wanaokimbia kutoka Ghouta mashariki. Amesema majeshi ya Uturuki na Urusi yatashirikiana kujenga hospitali hiyo.
Kwa upande wake rais Donald Trump ambaye nchi yake hakualikwa kuhudhuria mkutano wa nchi tatu zinazohusika katika mzozo wa Syria amekubali katika kikao cha baraza la usalama la taifa kuendelea kuviweka vikosi vya majeshi ya nchi hiyo nchini Syria kwa muda zaidi lakini anataka viondoke haraka iwezekanavyo, amesema afisa mwandamizi wa utawala huo leo.
Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umesema leo kwamba umepeleka ujumbe wake wa kwanza wa kiutu mjini Raqa tangu mji huo wa Syria kukombolewa kutoka udhibiti wa kundi la Dola la Kiislamu, ukionya kwamba raia wanaorejea wanakabiliwa na mzigo mkubwa. Mji huo ambao kundi la IS liliutangaza kuwa sehemu ya utawala wake wa kikhalifa mwaka 2014, umetapakaa mabomu ambayo hayaja ripuka, mkuu wa ujumbe wa kutoa misaada ya kiutu wa Umoja wa mataifa nchini Syria , Jan Egeland aliwaambia waandishi habari mjini Geneva leo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre/ afpe / dpae
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman