Mkutano wa uhai anuai wafungwa rasmi Bonn
30 Mei 2008Kiasi ya wajumbe 6,000 kutoka nchi 191,waliokusanyika Bonn hasa wamejadiliana njia ya kutekeleza maamuzi ya mkutano huo,hadi ifikapo mwaka 2010.Njia ya kukomesha uharibifu wa misitu pamoja na mimea na viumbe vya misitu hiyo ni mada iliyopewa kipaumbele.
Suala jingine lililopewa umuhimu ni kile kilichoitwa "uharamia wa kimaumbile"-kwa mfano,viwanda vya kutengeneza dawa vinapochukua mitishamba kutoka nchi masikini bila ya idhini ya wenyeji au bila ya kuwalipa fidia.Kwani nchi hizo masikini zenye utajiri wa maliasili zina wasi wasi na viwanda vinavyoandikisha hakimiliki ya mitishamba kwa jina lao na hao wanaomiliki maliasili na ujuzi wa mitishamba hawalipwi hata senti moja.
Kwa hivyo makubaliano yalioitwa "Mwongozo wa Bonn" juu ya njia ya kugawana faida zinazotokana na maliasili ni fanikio kuu pekee katika mkutano huo wa Bonn.Mkuu wa Miradi ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa UNEP,Achim Steiner amesema:
"Tuna upepo mpya unaovuma katika mkutano huu.Na umefikia kilele chake.Kutokana na majadiliano haya tumeweza kushuhudia kwa wakati mmoja inamaanisha nini pale mtu anapofungua mlango na kunyosha mkono kuwasaidia zaidi wengine."
Suala la uhai anuai linajadiliwa tangu miaka kumi na sita iliyopita,kwa hivyo wajumbe mkutanoni wamekubali kuwa sasa wakati umewadia kuweka malengo yatakayosaidia kupunguza kasi ya uteketezaji wa mimea na viumbe hadi ifikapo mwaka 2010.
Ujerumani imeahidi kutoa kiasi cha Euro milioni 500 kati ya mwaka 2009 na 2012,kusaidia kuhifadhi mimea na viumbe vilivyo katika hatari ya kutoweka.Na kuanzia 2013 Euro milioni 500 zingine zitatolewa kila mwaka kusaidia mradi huo.