Mkutano wa umoja wa Afrika waanza
19 Julai 2010Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika unafunguliwa leo hii mjini Kampala Uganda huku kukiwa na ulinzi mkali kufuatia mashambulizi mawili ya mabomu mjini humo wiki iliopita.Mada rasmi iliokuwa imepangwa kuhodhi mkutano huo vifo va watoto wachanga na vifo vinavyotokana na uzazi yumkini ikatiwa kiwingu na mjadala juu ya shughuli za kulinda amani za Umoja wa Afrika nchini Somalia.
Miripuko hiyo ya mabomu ambayo imeuwa zaidi ya watu 70 na kujeruhi wengine zaidi ya 80 wakati walipokuwa wakiangalia fainali za michuano ya soka Kombe la Dunia katika mkahawa mmoja wa Kihabeshi na katika viwanja va raga kwenye vitongoji vya mji wa Kampala wiki iliopita.
Mashambulizi hayo yamekuja ikiwa ni siku mbili tu baada ya msemaji wa kundi la al-Shabab nchini Somalia ambalo linapambana na serikali dhaifu ya mpito nchini humo kusema kwamba Uganda itashambuliwa kutokana na dhima yake katika mzozo wa Somalia.
Uganda ina wanajeshi wengi kati ya wanajeshi takriban 6,000 wa Umoja wa Afrika (AMISOM) walioko nchini Somalia kuilinda serikali ya mpito ya nchi hiyo inayoshikilia baadhi ya maeneo ya mji mkuu wa Mogadishu.
Kufuatia mashambulizi ya Kampala msemaji huyo wa al-Shabab Ali Mohamoud Rage amesema wanatuma ujumbe kwa kila nchi ambazo zina nia ya kupeleka wanajeshi wake nchini Somalia kwamba zitashambuliwa ndani ya nchi zao na kuongeza kwamba Burundi ambayo ina wanajeshi wake katika kikosi hicho cha AMISOM pia itashambuliwa iwapo haitowandowa kutoka Somalia.
(Bahoku Barigye msemaji wa kikosi cha AMISOM ameliambia shirika la habari la IPS kwamba wana vikosi vinavyolinda uwanja wa ndege,kasri la rais, bandari na vituo vyengine muhimu n kubakiwa na wanajeshi wachache wa kuwalinda raia kwa hiyo wanahitaji wanajeshi zaidi.
Watu 20 wametiwa mbaroni nchini Uganda na wawili wamekamatwa nchini Kenya kwa kuhusika na mashambulizi hayo.)
Lakini baadhi ya wachambuzi wanasema kuongeza kwa wanajeshi hakutosaidia kitu kwa kutowa mfano wa matatizo yaliowakabili wanajeshi wa Ethiopia walioingia Somalia hapo mwezi wa Desemba mwaka 2006 kulitimuwa kundi la itikadi kali za Kiislam la Umoja wa Mahkama za Kiislam lillilokuwa likitaka kuanzisha utawala wa sheria za Kiislam Sharia nchini Somalia.
Ingawa harakati za Umoja wa Mahkama za Kiislam kuidhibiti Somalia zilikomeshwa kikosi cha Ethiopia hakikuweza kuuteka kikamilifu mji mkuu wa Mogadishu au kuweka udhibiti nje ya mji huo na hiyo kilijitowa nchini humo na nafasi yake kuchukuliwa na kikosi cha Umoja wa Afrika AMISOM.
Mtaalamu wa siasa wa Chuo Kikuu cha Makerere Yassin Olun anaamini kwamba wakati umefika kwa Uganda kuangalia upya msimamo wake nchini Somalia kwa nia ya kujitowa nchini humo.
Olum amesema inabidi wajiulize kwa nini nchi za Kiafrika hazipeleki vikosi vyake nchini Somalia huenda kwamba wamen'amuwa kwamba ni kumoto au wanaona kwamba hilo ni suala la ndani ya nchi.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema wanajeshi zaidi wanatakiwa kutumwa Somalia hadi kufikia 20,000 na amedokeza kwamba Uganda itapeleka wanajeshi wake zaidi iwapo nchi nyengine hazitokuwa tayari kufanya hivyo.
Pia ameihakikishia Marekani ambayo ina utashi zaidi wa harakati za itikadi kali za Kiislam nchini Somalia kwamba Uganda haitojiengua na mzozo wa Somalia.
Balozi wa Marekani nchini Uganda Jerry Lanier amesema Marekani inapanga kuongeza msaada kwa Uganda na kwa kikosi cha AMISOM.
Kuna wasi wasi kwamba ingawa mada ya mkutano huo wa Kilele wa Umoja wa Afrika mjini Kampala ni Afya ya Uzazi ,Watoto na Maendeleo barani Afrika kutiliwa maani kwa malengo hayo ya maendeleo yumkini kukapata pigo kama ilivyokuwa kwa mada zilizopita za maji, ushughulikiaji wa maji taka na kukuza kilimo. Bila ya shaka azmio litatolewa lakini mkutano huo utatawaliwa na mashambulizi ya al- Shabab nchini Uganda.
Mwandishi:Mohamed Dahman/IPS
Mhariri: Muni ra Muhammad