Mkutano wa umoja wa Afrika wajaribu kuepuka mgawanyiko kuhusu Zimbabwe.
1 Julai 2008
Mkutano wa umoja wa Afrika mjini Sharm El Sheikh nchini Misr leo umekuwa ukijaribu kujiepusha na mgawanyiko juu ya vipi viongozi wa nchi hizo wanaweza kulishughulikia suala la kuchaguliwa tena rais Robert Mugabe katika uchaguzi ambao umeshutumiwa duniani kote.
Sekione Kitojo anaichunguza hali hiyo.
Duru katika mkutano huo zinasema kuwa viongozi wamegawanyika baina ya wale ambao wanataka kutoa matamshi makali juu ya Zimbabwe na wengine ambao wanasita sita kutoa matamshi hayo hadharani na kumshutumu kiongozi huyo mkongwe, ambaye amerefusha utawala wake wa miaka 28 katika uchaguzi ambapo alikuwa mgombea pekee Ijumaa iliyopita.
Rais wa Sierra Leone , Ernest Bai Koroma , ambaye ni mmoja kati ya kundi la viongozi wa mataifa ya Afrika magharibi na mashariki ambao ni wakosoaji wakubwa wa rais Mugabe, amesema kuwa watu wa Zimbabwe wamenyimwa haki yao ya kidemokrasia. Tunapaswa, bila kujali chochote kushutumu kile kilichotokea.
Koroma amesema kuwa kundi la mataifa ya kusini mwa Afrika ni lazima wawashirikishe Mugabe na Tsvangirai , ambaye alijitoa katika uchaguzi kutokana na kushambuliwa na vitisho dhidi ya wafuasi wa chama chake, katika mazungumzo yatakayoleta serikali ya mpito pamoja na uchaguzi mpya.
Lakini msemaji wa rais Mugabe George Charamba amekataa wazo la kuwa na suluhisho kama la Kenya la kuwa na mpango wa kugawana madaraka serikalini, mpango ambao umedokezwa na viongozi kadha katika mkutano wa viongozi wa Afrika, ili kumaliza mzozo ambao umeikabili Zimbabwe pamoja na hali mbaya ya kiuchumi pamoja na mataifa ya jirani kutaabika kuwahifadhi mamilioni ya wakimbizi katika nchi zao.Katika shutuma zake Charamba amemlenga zaidi waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga.
Chama cha Movement for Democratic Change kimepinga ripoti moja ya gazeti la Afrika kusini kuwa mpatanishi mkuu wa mzozo wa Zimbabwe rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini alikuwa yuko karibu na kupata makubaliano kutoka kambi ya Mugabe na Tsvangirai kuweza kujadili kuhusu serikali ya umoja wa kitaifa.
Katibu mkuu wa chama cha MDC Tendai Biti , ambaye ametoka kifungo kwa dhamana kuhusiana na kesi ya uhaini dhidi yake, amesema kuwa ukweli ni kwamba hakuna mazungumzo yoyote ama majadiliano yanayofanyika baina ya pande hizi mbili na muhimu zaidi , hakuna makubaliano yoyote yanayotarajiwa.
Biti amesema kuwa wakati chama cha MDC kilikuwa kinatafuta njia ya majadiliano katika juhudi za kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kabla ya Juni 4, uchaguzi wa bandia uliofanyika wa duru ya pili Juni 27, umeondoa kabisa uwezekano wowote wa kupata suluhisho kwa njia ya majadiliano.
►◄