1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa umoja wa Ulaya na mataifa ya Afrika kuhusu EPA waingia mtafaruku.

Sekione Kitojo11 Novemba 2007

Wakati mkesha wa muda wa mwisho wa kukamilishwa kwa makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi baina ya mataifa ya Afrika na Ulaya unakaribia kinachotawala hivi sasa ni majadiliano na mtafaruku wa mambo.

Mawaziri wa kundi la mataifa ya mashariki na kusini mwa Afrika wanakusanyika mjini Brussels, nchini Ubelgiji , wiki hii kwa majadiliano na umoja wa Ulaya . Ni suala la kungoja na kuona iwapo mazungumzo hayo yatakwama na kusogezwa mbele hadi mwaka ujao, ama iwapo utakubalika mkataba unaojulikana kama mkataba mwepesi wa EPA. Mkataba mwepesi wa EPA , unamaana ya makubaliano ya muda yanayogusa mada mbili, kwa upande mmoja , mataifa ya Afrika kuweza kutumia soko la umoja wa Ulaya kwa bidhaa zake na upande wa pili maendeleo.

Kuna mtafaruku katika maeneo mawili. Kwanza , nchi hizi 16 za kundi la ESA, katika wakati huu, yanagawiwa katika sehemu mbili, na kuyaingiza majadiliano katika mtafaruku mkubwa. Jumuiya ya Afrika mashariki ambayo inaundwa na Kenya, Tanzania, Uganda, Burundi, na Rwanda zina umoja wao wa forodha na umeamua kutia saini makubalino yao ya pekee ya EPA na umoja wa Ulaya.

Mataifa yaliyoko katika bahari ya Hindi, Mauritius, Seychelles, Madagascar na Comoro pia yameamua kujadiliana mkataba wa pekee wa EPA. Mataifa haya yametumia miaka miwili iliyopita yakijadili na umoja wa Ulaya waraka wa pamoja na EPA. Haifahamiki wazi vipi nyaraka mpya zinaweza kufungwa pamoja katika muda mfupi uliopo kabla ya muda wa mwisho , mwishoni mwa mwaka huu.

Kubadilika kwa sura ya makundi ya nchi kwa ajili ya majadiliano hata sio tatizo kubwa. Kuna tofauti kubwa bado baina ya umoja wa Ulaya na nchi zinazounda ESA katika masuala ya msingi sana. Kwanza kabisa , hakujakuwa na makubaliano ya kimawazo juu ya nini maana ya maendeleo. Pande zote mbili umoja wa Ulaya na mataifa ya Afrika zimekubaliana kuwa maendeleo ndio uwe uti wa mgongo wa majadiliano ya EPA. Lakini hata hivyo pande zote mbili zinatofautiana pa kubwa katika tafsiri ya kile kinachomaanishwa katika hali halisi.

Nchi za ESA zinatoa tafsiri ya maendeleo kama uimarishaji wa msingi wao wa viwanda na kilimo, na wamekuwa wakitoa mbinyo kwa umoja wa Ulaya kuahidi kukubaliana na orodha ya miradi ya maendeleo pamoja na ahadi za kusaidia miradi hiyo.

Umoja wa Ulaya haujapendelea suala hilo na imekuwa ikijaribu kuweka kando masharti hayo. Umoja wa Ulaya umefanikiwa kulishawishi kundi la ESA kupunguza madai yao.

Kwa mujibu wa Jane Nalunga wa asasi isiyo ya kiserikali ya taasisi ya mashariki na kusini mwa Afrika ya majadiliano na taarifa za biashara, SEATINI, amesema kuwa wakati tulipopata muswada wa waraka wa majadiliano, tuliweka kipengee cha maendeleo. Umoja wa Ulaya ukasema hapana , tukiondoe.

Hawakusema kuanzia mwanzo kuwa , hawatakifikiria. Wamesema kiondoeni na kiwekeni katika eneo la yatokanayo. Tutakihusisha katika waraka baadaye. Hivi sasa kwa kuwa tumekiondoa, wanasema hii ni orodha ya manunuzi ya zawadi za krismass. Hawataki hata kuhusisha kipengee hicho kutoka yatokanayo katika waraka.