1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Umoja wa Ulaya waanza Lithuania

28 Novemba 2013

Mkutano wa Umoja wa Ulaya uliopangwa kuzivuta nchi sita zilizokuwa katika iliyokuwa Umoja wa Kisovieti kuelekea upande wa mataifa ya Ulaya unaaza rasmi leo mjini Vilnius nchini Lithuania.

epa03929896 Activists of Ukrainian public movement _For European future_ take part in rally on the Independence square in Kiev, Ukraine, 30 October 2013. Demonstrators announced the start of a campaign for a referendum about European choice of Ukraine. Ukraine can sign the Association Agreement with EU during Vilnius summit at November 2013. EPA/SERGEY DOLZHENKO
Wanaharakati wakionesha bendera ya ushirika na Umoja wa UlayaPicha: Picture-alliance/dpa

Nia ya mataifa hayo imepata pigo, baada ya Ukraine , moja kati ya nchi kubwa miongoni mwa nchi hizo sita, kujiweka karibu na Urusi na kusema hapana kusogeleana na mataifa ya Umoja wa Ulaya.

Wakati rais wa Ukraine Viktor Yanukovich atakapokabiliana na viongozi wa Umoja wa Ulaya katika mkutano huo wa ushirika na mataifa ya mashariki mjini Vilnius leo,(28.11.2013) hali haitakuwa ya kupendeza. Yanukovich ameweka wazi kuwa hayuko tayari kutia saini makubaliano ya kibiashara na kundi hilo la mataifa lenye wanachama 28, ambalo lilikuwa lengo kuu la Umoja huo.

Waandamanaji wanaotaka ushirika na Umoja wa UlayaPicha: Picture-alliance/dpa

Badala yake , amesema katika mahojiano yaliyotangazwa jana Jumatano kuwa anaamini uhusiano wa aina hiyo kati ya nchi yake na Umoja wa Ulaya ni mapema mno na kwamba anatarajia kuwa Urusi itafurahia msimamo huu na kuipa mikopo mipya serikali yake inayokabiliwa na matatizo ya kifedha.

Lawama dhidi ya Urusi

Maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya wametoa lawama kwa Urusi. Rais wa Lithuania Dalia Grybauskaite ameishutumu wazi Urusi kwa kuirubuni Ukraine.

Urusi haikukana tu shutuma hizo , lakini pia imesema ni Umoja wa Ulaya ambao unaiwekea mbinyo Ukraine. Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi amekwenda umbali wa hata kudokeza kuwa Umoja huo unachochea maandamano ya kuipinga serikali ambayo yameikumba Ukraine baada ya serikali kutangaza wiki iliyopita kwamba inasitisha matayarisho kuhusiana na makubaliano na Umoja wa Ulaya.

Rais wa Ukraine Viktor JanukovychPicha: picture alliance / AP Photo

Hata hivyo , rais Vladimir Putin wiki hii amekiri wazi kuwa Urusi ina maslahi makubwa ya kiuchumi kwa kuiweka Ukraine mbali na kutia saini makubaliano na Umoja wa Ulaya.

Akizungumza na waandishi habari wakati wa ziara yake nchini Italia, amedai kuwa hatua hiyo si tu kwamba itafanya bidhaa za Ukraine kuwa ghali nchini Urusi lakini hata bidhaa za mataifa ya Ulaya zitakazopelekwa nchini Urusi kupitia nchi hiyo.

Uwezekano bado upo

Rais wa Ukraine Viktor Yanukovich ameahidi pamoja na hayo kuwa atajiunga na viongozi wa mataifa 28 ya Umoja wa Ulaya katika mkutano unaoanza leo wa siku mbili katika mji mkuu wa Lithuania , Vilnius , moja kati ya nchi kadha zilizokuwa katika Umoja wa Kisovieti ambazo zimejiunga na Umoja wa Ulaya na zinataka kupanua wigo wa ushawishi wa kundi hilo la mataifa kuelekea upande wa mashariki.

Ukraine imesema jana kuwa bado inataka kufikia makubaliano ya kihistoria yanayohusu mahusiano ya karibu na Umoja wa Ulaya, wakati maandamano ya umma kuhusiana na hatua ya serikali kusitisha utiaji saini makubaliano hayo yakiingia katika siku ya nne.

Picha ya Julia Tymoschenko katika fulana ya muandamanajiPicha: picture-alliance/dpa

Kiongozi wa upinzani ambaye yuko kifungoni nchini Ukraine Yulia Tymoshenko amewatolea wito viongozi wa Umoja wa Ulaya kuacha madai yao yote na kutia saini makubaliano hayo ya kihistoria na ukraine bila ya kuweka masharti katika mkutano huo.

Umoja wa Ulaya umedai kuwa Ukraine iimarishe utawala wa sheria na kumuacha huru waziri mkuu huyo wa zamani ambaye yuko kifungoni kabla ya pande hizo mbili kutia saini makubaliano hayo ya kihistoria ya kisiasa na biashara huru.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW