1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa UN kujadili tena malengo ya maendeleo endelevu

18 Septemba 2023

Viongozi wakuu wa dunia wanaelekea New York, Marekani kushiriki mkutano wa Umoja wa Mataifa, wakati umoja huo ukijitahidi kusonga mbele na utekelezaji wa malengo muhimu ya maendeleo endelevu. Lakini maendeleo yanadorora.

New York I Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuanza mjini New York, Septemba 19, 2023.Picha: Michael M. Santiago/Getty Images

Ahadi zilikuwa kubwa na zenye malengo makubwa. Miongoni mwake: Kukomesha umaskini uliokithiri na njaa. Kuhakikisha kila mtoto duniani anapata elimu bora ya sekondari. Kufikia usawa wa kijinsia. Kupiga hatua muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kurahisisha upatikanaji wa nishati nafuu, ya kuaminika, endelevu na ya kisasa kwa wote, na kufikia haya yote ifikapo 2030.

Lakini katikati mwa safari ya kuelekea lengo hilo, maendeleo yanadorora, na baadhi ya wakati kurudi nyuma.

Katika mkutano wa kilele wa siku mbili unaoanza leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres atajaribu kuanzisha hatua za kufikia malengo 17 yaliyopitishwa na viongozi wa dunia mwaka 2015, ambayo nchi zinazoendelea hasa zinayaona kuwa muhimu katika kuziba pengo linaloongezeka la ukosefu wa usawa kati ya mataifa zajiri na maskini ya dunia.

Soma pia: Kikao cha misaada ya kibinadamu chafanyika Nairobi

Malengo hayo, Guterres alisema, ni "kuhusu kurekebisha makosa ya kihistoria, kuponya migawanyiko na kuweka ulimwengu wetu kwenye njia ya amani ya kudumu."

Tamko la kisiasa la kurasa 10 litakalopitishwa na viongozi mwanzoni mwa mkutano huo linatambua kuwa malengo "yamo hatarini" na linaonyesha wasiwasi kwamba maendeleo yanakwenda polepole sana au yanarudi kwa viwango vya kabla ya 2015.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amesema ni wakati wa kurejesha SDGs kwenye njia ya utekelezaji.Picha: Yuki Iwamura/AFP/Getty Images

Linathibitisha tena zaidi ya mara kumi na mbili, kwa njia tofauti, kujitolea kwa viongozi kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu, au SDGs, na kusisitiza umuhimu wa kila lengo. Hii inawezaje kufanywa katika miaka saba ijayo?

Tamko linalokosa ufafanuzi

Viongozi hao wamejitolea kuharakisha hatua. Lakini tamko wanalofanya kazi nalo linakosa ufafanuzi wa hatua makhsusi.

Mwanzoni mwa "Wikendi ya Hatua ya SDG," siku ya Jumamosi, Guterres aliwapitisha wanaharakati katika matokeo ya kusikitisha ya ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwezi Julai: Ni asilimia 15 tu ya baadhi ya malengo 140 mahususi ya kufikia malengo 17 yaliotimizwa. Mengi yako kwenye mwelekeo mbaya.

Katika kiwango cha sasa, ripoti ilisema, watu milioni 575 bado watakuwa wanaishi katika umaskini uliokithiri na watoto milioni 84 hata hawataenda shule ya msingi mwaka 2030 - na itachukua miaka 286 kufikia usawa kati ya wanaume na wanawake.

"SDGs zinahitaji mpango wa uokoaji wa kimataifa," mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema. Aliuita mkutano huo "wakati kwa serikali kuja mezani na mipango madhubuti na mapendekezo ya kuharakisha maendeleo."

Sio serikali pekee zinazohitaji kukaza buti, Guterres alisema. Aliwataka wanaharakati pamoja na jumuiya ya wafanyabiashara, wanasayansi, wasomi, wavumbuzi, wanawake na vijana kuungana katika kufanya kazi ili kufikia malengo.

Mke wa Rais wa Marekani, Jill Biden, alimuunga mkono katibu mkuu katika tafrija ya Jumapili jioni iliyoandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, kwa mabingwa wa elimu duniani. Alisema maendeleo katika kufikia SDGs "yanaonekana kuwa mwinuko." Lakini alisema Marekani "itaendelea kuwa mshirika wenu kila hatua ya njia."

Moja ya malengo 17 ya Umoja wa Mataifa ni kuhakikisha upatikanaji salaama wa maji kote duniani.Picha: Caro Trappe/picture alliance

Kama mwalimu kwa miaka 39, bibi Biden alihimiza kila kiongozi wa nchi kuwekeza kwa watoto, akisema "watatusaidia kujenga dunia yenye amani na utulivu."

Mpango wa kuondoa vikwazo njiani

Guterres alisema mkakati muhimu zaidi wa kuokoa mpango wa jumla ni pendekezo la kile alichokiita "kichocheo cha SDG," ambacho kinalenga kukabiliana na hali ya soko yenye changamoto zinazoyakabili mataifa yanayoendelea.

Kichocheo hicho kinatoa wito wa hatua za haraka katika maeneo matatu, ambayo ni kukabiliana na gharama kubwa za madeni na hatari inayoongezeka ya dhiki ya madeni; kuongeza ufadhili wa muda mrefu wa maendeleo, hasa kutoka benki za umma na kimataifa; na kupanua ufadhili wa dharura kwa mataifa yenye uhitaji.

Soma pia: Maendeleo endelevu yapata ufadhili

Ripoti ya Februari ya Umoja wa Mataifa kuhusu Kichocheo cha SDG ilisema madeni yanadhoofisha uchumi wa nchi nyingi zinazoendelea. Ilisema hadi kufikia Novemba mwaka jana, nchi 37 kati ya nchi 69 maskini zaidi duniani zilikuwa katika hatari kubwa au tayari ziko kwenye dhiki ya madeni, huku moja kati ya nchi nne zenye kipato cha kati, ambazo zina watu wengi maskini waliokithiri, zilikuwa katika hatari kubwa ya kutumbukia katika mgogoro wa kifedha.

Kuna mwanga mdogo wa matumaini. Guterres alisema alitiwa moyo kuwa katika mkutano wa hivi karibuni wa G20, nchi 20 zinazoongoza kwa uchumi duniani zilikaribisha Kichocheo cha SDG. Na alisema ana matumaini kwamba tamko la kisiasa litakalopitishwa na viongozi siku ya Jumatatu litasababisha hatua kubwa.

Tamko hilo linasema viongozi watasukuma mbele mpango wa kichocheo "kukabiliana na gharama kubwa za madeni na kuongezeka kwa hatari ya dhiki ya madeni, kuongeza msaada kwa nchi zinazoendelea na kuongeza kwa kiasi kikubwa ufadhili wa muda mrefu wa maendeleo na kupanua ufadhili wa dharura kwa nchi maskini zenye uhitaji."

Ikiwa ahadi hizo za kiutawala na kasi ya wiki kubwa katika Umoja wa Mataifa itatafsiri katika maendeleo halisi, inasalia kuwa - kama hapo awali - jambo la mashaka makubwa.

Chanzo: Mashirika