1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwenyekiti MSC aitaka Ujerumani kuongeza matumizi ya kijeshi

20 Februari 2023

Mkutano wa kimataifa wa usalama wa Munich uliogubikwa na vita vya Urusi nchini Ukraine umemalizika. Mwenyekiti wake, mshauri wa zamani wa Angela Merkel, aliuhitimisha kwa kuitaka Ujerumani kuongeza matumizi ya kijeshi.

Münchner Sicherheitskonferenz
Picha: Sven Hoppe/dpa/picture alliance

Mwenyekiti mpya wa Mkutano wa Usalama wa Munich, MSC, ni Christoph Heusgen, ambaye aliwahi kufanya kazi kama mshauri wa karibu wa kansela wa Ujerumani Angela Merkel, na pia kama balozi wa Ujerumani nchini Marekani.

Alihitimisha mkutano huo jana Jumapili akisema wazungumzaji mbalimbali walikuwa wamedhihirisha wazi kwamba Ulaya inapaswa kufanya kazi ili kuendelea kuimarisha umoja wa kanda ya Atlantiki, ambao alisema ulioneshwa wakati wote wa mkutano huo wa mwishoni mwa wiki.

Soma pia: Mkutano wa Munich wamalizika kwa miito ya kuisaidia Ukraine

Heusgen alisema matumizi ya kijeshi ya Ulaya na Ujerumani yanapaswa kuongezeka, na kuongeza kuwa ujumbe huu ulikuwa wa wazi zaidi wakati wa mkutano, akisisitiza haja ya kuwa na uwezo wa kuisadia Ukraine, lakini pia kujenga uwezo wao wa kijeshi.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen alikubaliana na rai hiyo ye mwenyekiti wa MSC kuhusu suala la kuisaidi Ukraine.

Waziri Mkuu wa Finland Sanna Marin, kushoto, na Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen wakizungumza kwenye Mkutano wa Usalama wa Munich mjini Munich, Ujerumani, Februari 17 hadi Februari 19, 2023.Picha: Petr David Josek/AP Photo/picture alliance

Akizungumza kwenye mkutano huo, Von der Leyen alipendekeza kwa kanda hiyo ifanye kile ilichokifanya wakati wa janga la Uviko, kujiandaa kwa uzalishaji mkubwa wa dawa za chanjo ya Uviko-19.

Von der Leyen alisisitiza kwamba kanda hiyo haiwezi kusubiri kwa miezi na miaka kuweza kujaza hifadhi yake ya kijeshi au kutuma silaha kama vile risasi za makombora za 155mm kwa Ukraine.

Soma pia: Zelenskyy ahimiza kupelekewa silaha haraka

"Nadhani sasa ni wakati wa kuharakisha uzalishaji na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za viwango ambazo Ukraine inazihitaji sana. Kwa mfano, risasi sanifu ... haiwezi kuwa kwamba tunasubiri miezi na miaka hadi tuweze kujaza tena, hadi tuwe na uwezo wa kuwasilisha vifaa hivyo kwa Ukraine."

China yaikosoa "madai ya uongo ya Marekani" kwamba inaweza kuisaidia Ukraine

Beijing imelani Jumatatu kile ilichokiita madai ya uongo yaliotolewa na Marekani kwamba nchi hiyo inapanga kuipatia Urusi silaha katika vita vyake dhidi ya Ukraine.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Wang Wenbin amesema ni Marekani na siyo China inayoendelea kusaifirisha silaha kwenye uwanja wa vita, na kuitaka nchi hiyo kutafakari matendo yake yenyewe, na kufanya zaidi ili kutuliza hali, kukuza amani na majadiliano, na kuacha kuhamisha lawama na kueneza taarifa za uongo.

Waziri wa Mambo y aNje wa China Wang Yi, kushoto, akihojiwa na Balozi Wolfgang Ischinger, wakati wa Mkutano wa Usalama wa Munich, Februari 18, 2023, mjini Munich, Ujerumani.Picha: Lukas Bar/ZUMA/IMAGO

Soma pia: Mkutano wa kimataifa wa usalama kuanza Munich

Taarifa hiyo ya China imekuja baada ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, kukiambia kituo cha utanagazaji cha CBS katika mahiojiano kwamba China sasa inazingatia kutoka msaada wa kijeshi kwa Moscow, kuanzia risasi hadi silaha zenyewe.

Alitoa matamshi sawa na hayo katika mfululizo wa mahojiano nchini Ujerumani, ambapo siku ya Jumamosi alihudhuria Mkutano wa Usalama wa Munich na kukutana na mwenzake wa China, Wang Yi.

Shutuma za Blinken zilikuja wakati uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ukiwa umedorora zaidi baada ya Washington kudungua kile ilichosema ni puto ya kijasusi la China.

Kumekuwa na wasiwasi kwamba China inazidisha uhusiano na Urusi licha ya mzozo huo -- lakini Wang Yi alisema Beijing ilikuwa na jukumu la kujenga, na kusimama kidete upande wa mazungumzo.

Chanzo: Mashirika, DW