Mkutano wa uwekezaji Afrika wafanyika Berlin
20 Novemba 2023Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amewaalika viongozi wa mataifa ya Kiafrika na yaliyostawi kiviwanda ya kundi la G20. Mpango huo ulianzishwa na Ujerumani wakati ikiwa mwenyekiti wa kundi hilo mwaka wa 2017 na unalenga kukuza uwezekaji zaidi wa kibinafsi katika mataifa ya Kafrika ili kuupiga jeki uchumi wao.
Soma pia: Ujerumani kufanya biashara ya nishati na Nigeria
Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Robert Habeck pia anahudhuria mkutano huo wa kilele, pamoja na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, viongozi kumi wa mataufa ya Kiafrika na serikali, na zaidi ya mawaziri 30 kutoka barani humo.
Heiko Schwiderowski, mkuu wa Chama cha Viwanda na Biashara cha Ujerumani anayehusika na masuala ya kanda ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, DIHK, anasema nia ya mpango huo wa ushirikiano na Afrika imeongezeka. Anasisitiza kuwa kongamano hilo la uwekezaji lenye wajumbe 800 linaelezewa kuwa kongamano kubwa kabisa la kibiashara kuwahi kufanyika kwenye ardhi ya Ujerumani.
Schwiderowski anasema viongozi wa kibiashara na kisiasa nchini Ujerumani wanatuma ishara muhimu, akiongeza kuwa kupanua mahusiano ya kiuchumi ni jitihada yenye manufaa.
Je, mpango huo umeleta mafanikio Afrika?
Mchambuzi kutoka Ghana Emmanuel Bendah anasema mipango kama hii ya ushirikiano wa G20 na Afrika ni nyenzo muhimu cha kutathmini uchumi wa Afrika na pia kutumika kama kifaa cha kupima maendeleo ya nchi za bara hilo, kwa sababu inawezesha kupata picha za nchi tofauti na kuona kinachoendelea nchini humo na kinachotatikana kuimarishwa.
XN Iraki, profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Nairobi anayehusika na ukuaji uchumi, anasema bado ni mapema mno kufanya tathmini ya mradi huo. Anasema ni wazo zuri lakini miaka sita ni michache mno kujua athari zake. Profesa huyo anasema mazingira barani Afrika sio mazuri kwa uwekezaji wa kibinafsi.
Iraki anasema Afrika haina miundo mbinu mizuri, kuna ukosefu wa utulivu wa kisiasa, na Imani kuwa nchi za Kiafrika zinahitaji kusaidiwa na mwingine. Hata hivyo anaamini kuwa ni muda mwafaka kwa nchi za Kiafrika kuchukua jukumu Zaidi.
Mtalaamu wa kiuchumi kutoka Ujerumani Robert Kappel ana mtizamo wa tahadhari. Ameiambia DW kuwa ipo haja ya kuufanyia mabadiliko muundo huo na kuangazia Zaidi ukweli kuwa maslahi ya Afrika yana jukumu kubwa. Maslahi ya Afrika yanajikita katika utanuzi wa viwanda na utengenezaji wa ajira.
Soma pia: Kansela Angela Merkel ahimiza uwekezaji barani Afrika
Kiasi ya mataifa 13 ya Kiafrika mpaka sasa yameungana katika mpango huo, Benin, Burkina Faso, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia, Misri, Ethiopia, Ghana, Guinea, Morocco, Rwanda, Senegal, Togo na Tunisia. Kama mojawapo ya nchi kubwa kiuchumi barani Afrika, Afrika Kusini inashikilia uwenyekiti mwenza wa kongamano hilo.
Nchi nyingine kama vile Angola, Zambia, Nigeria na Kenya zinahudhuria kongamano hilo la Berlin kama wageni.
Makala hii ilitafsiriwa kutoka Kijerumani