1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa viongozi wa G7 na Umuhimu wake duniani

Oumilkheir Hamidou
26 Agosti 2019

Mkutano wa viongozi wa mataifa saba yaliyoendelea kiviwanda G-7 mjini Biarritz nchini Ufaransa, na hofu AfD wasije wakaibuka na ushindi Uchaguzi utakapoitishwa jimboni Brandenburg ni miongoni mwa mada magazetini.

G7-Gipfel in Frankreich
Picha: Reuters/C. Barria

Tunaanza lakini na mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa saba yaliyoendelea zaidi kiviwanda ulimwenguni G-7. Kama ilivyoshuhudiwa katika mkutano kama huo ulioitishwa Canada mwaka jana, na katika huu pia wa mjini Biarritz nchini Ufaransa, hakuna la muhimu lililofikiwa. Wahariri wanajiuliza kama kweli kuna haja ya kuiendeleza mikutano ya G-7.Gazeti la Reutlinger General-Anzeiger linaandika: "Licha ya hitilafu zote za maoni ni muhumu kuhakikisha mikutano ya kilele ya G-7-inaendelea kuitishwa. Kwanza kwasababu  kuna siku itafikia tu ambapo enzi za Trump zitamalizika. Na pili kutoiendeleza mikutano hiyo itamaanisha kusalim amri.

Mataifa sita yaliyosalia miongoni mwa saba yaliyoendelea zaidi kiviwanda yanabidi yajitahidi, hata bila ya dola kuu la Marekani, kufikia makubaliano. Ishara ya nguvu upande huo ilikuwa kualikwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran. Trump aliudhika sana kwasababu Marekani inaiangalia Iran kuwa ni adui. Lakini mataifa sita yaliyosalia au G6 wana lengo jengine. Wanataka kuyanusuru makubaliano ya mradi wa nuklea wa Iran, wanataka kuendeleza biashara na kuepusha balaa la kuzuka vita. Rais wa Ufaransa amebainisha, watu wasikubali kufuata amri ya Donald Trump."

Kitisho cha AfD kuingia madarakani Brandenburg

Septemba mosi inayokuja, wapigakura wa jimbo la mashariki la Brandeburg watateremeka vituoni kulichagua bunge jipya. Wasi wasi umeenea miongoni mwa vyama vya jadi, CDU na SPD na pia chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto die Linke visije vikaondoka patupu jumapili inayokuja. Wanaopigiwa upatu wa kuibuka na ushindi ni wale wa chama kinachopinga wageni "Chaguo Mbadala kwaajili ya Ujerumani" AfD. Hata hivyo maajabu yanaweza pia kutokea, anaandika mhariri wa gazeti la  mjini Berlin la "Morgen Post" anaewazungumzia wale ambao mpaka sasa bado hawajaamua watapiga kura upande gani: "Kusema kweli, sijaamua bado nani nitampigia kura jumapili inayokuja.Uchaguzi kweli unaitishwa lakini sijawahi kupata shida ya kuamua kama safari hii. Hasa kwasababu safari hii kuna suala muhimu linalojitokeza nalo ni kama mji jirani na Berlin uachiwe kuangukia mikononi mwa AfD au kama iundwe serikali ya muunganmo ambayo lengo kuu ni kuwafungia milango AfD. Ukweli  halisi wa mambo hakuna anaeuzingatia."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga