1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa viongozi wa G7 waanza Ufaransa

15 Juni 2026

Viongozi wa mataifa yanayoongoza kwa uchumi wa viwanda (G7) wanakusanyika nchini Ufaransa kwa mkutano wa kilele unaofunikwa na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran na vile vya Urusi dhidi ya Ukraine.

G7-Gipfel 2026 | Bilaterales Treffen zwischen Donald Trump & Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alipokutana na mwenzake wa Marekani Donald Trump pembezoni mwa mkutano wa G7 unaofanyika UfaransaPicha: Julia Demaree Nikhinson/AP Photo/picture alliance

Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye amekuwa na majibizano makali na mwenyeji wa mkutano huo, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, anahudhuria kusanyiko hilo la mataifa yenye nguvu duniani akitembea kifua mbele kwa kile anachoamini ni kufanikisha makubaliano ya kuelekea mkataba wa kukomesha vita alivyovianzisha mwenyewe na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, mwishoni mwa mwezi Februari dhidi ya Iran, na ambavyo vilikuja kugeuka kuwa janga la ulimwengu mzima.

Tafauti ya kimtazamo juu ya vita hivyo haikuwa kati ya Trump na Macron tu, bali pia na washirika wa kijadi wa Marekani kwenye kundi hilo la G7, kama vile Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani na hata Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, wote kwa nyakati tafauti walikataa kumuunga mkono kwenye vita vyake hivyo, wakimshutumu kwa kuchukuwa hatua hiyo kubwa bila kuwashauri.

Matokeo yake, Trump ametishia kuzichukulia hatua nchi hizo, ikiwemo kupunguza idadi ya wanajeshi wa Marekani kwenye nchi zote nne, ambazo kwa upande mwengine zote ni wanachama wa Muungano wa Kijeshi wa NATO.

Macron ataka Trump asaidie kumaliza vita Ukraine

Licha ya kutafautiana kwenye vita dhidi ya Iran, Rais Macron alisema tangu awali kwamba angeliutumia mkutano huu wa kilele kusaka uungaji mkono wa Trump kwa Ukraine na kuongeza mbinyo zaidi kwa Urusi ili kusaidia kwenye kupatikana mkataba wa amani. 

Rais Donald Trump wa Marekani akipanda ndege mjini Maryland kuelekea kwenye mkutano wa G7 nchini Ufaransa siku ya Jumatatu (Juni 15).Picha: Julia Demaree Nikhinson/AP Photo/dpa/picture alliance

Akizungumza na kituo cha utangazaji cha Ufaransa cha TF1 siku ya Jumatatu, Macron alisema "Tunaitaka Marekani alisema: 'Tuko pamoja nanyi, tutaendelea kuisaidia Ukraine, na tutazidisha shinikizo dhidi ya Urusi ili kupata majadiliano yenye maana. Majadiliano hayo ni yale ambayo Ukraine na Urusi zinakaa pamoja kitako, lakini pia Wamarekani na watu wa Ulaya wakiwepo."

Wakati Trump alitarajiwa kuwasili nchini Ufaransa na kukutana na Macron siku ya Jumatatu (Juni 15), Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine  alitazamiwa kuwasili na kuungana nao siku ya Jumanne.

Kwa upande mwengine, Macron alisema hatarudi nyuma licha ya kitisho cha Trump kuiwekea Ufaransa ushuru wa asilimia 100 kwa mvinyo wake, hadi pale Ufaransa itakapoondosha ushuru wa dijitali kwa kampuni za Marekani. 

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa akizungumza na wafanyakazi wa kikosi cha ulinzi kabla ya kufanyika mkutano wa kilele wa mataifa ya G7 katika mji wa Evian-les-Bains siku ya Jumatatu (Juni 15).Picha: Christian Hartmann/AP Photo/picture alliance

"Tunachotaka kukionesha ni kwamba ushuru haumfaidishi yeyote, hasa baina ya nchi wanachama wa G7. Haufaidishi sekta ya uchumi. Hauifaidishi hata Marekani yenywe, kwa kuwa hautatuwi matatizo yao ya kiuchumi na wanaongeza tu bei." Alisema Macron.

Mbali ya Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uingereza, kundi la mataifa hayo saba yenye nguvu za viwanda ulimwenguni linazijumuisha pia Canada na Japan na, kwenye mkutano huu wa kilele, zimealikwa pia Brazil, Misri, India, Kenya, Korea Kusini, Qatar, Syria, Ukraine, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW