Mkutano wa Beijing.
24 Oktoba 2008Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ametoa mwito juu ya kuimarisha wajibu wa shirika la fedha la kimataifa IMF ,katika nyakati hizi ngumu ambapo dunia inakabiliwa na mgogoro wa fedha.
Kansela Merkel amesema hayo leo kwenye mkutano wa viongozi wa Ulaya na bara la Asia unaofanyika mjini Beijing kujadili mgogoro huo.
Kansela Merkel amesema dunia sasa inahitaji kuwa na utaratibu mzuri. Ameeleza kuwa hayo yana maana ya kuimarisha wajibu wa shirika la fedha la kimataifa IMF, katika kuleta utengemavu katika mfumo wa fedha duniani.
Kiongozi huyo wa Ujerumani anaehudhuria mkutano wa kilele wa viongozi wa Ulaya na wa nchi za jumuiya ya Asem mjini Beijing pia ametoa mwito juu ya kuwapo uwazi na taratibu imara katika kudhibiti mosoko ya fedha , ili kusaidia katika juhudi za kuukabili mgogoro wa fedha uliopo sasa.
Viongozi hao kutoka Ulaya na nchi za Asia pia wanajadili njia za kukabiliana na mgogoro wa fedha ambao pia umezikumba nchi za Asia.
Akifungua mkutano huo leo, rais Hu Jintao wa China amesema, mgogoro wa fedha ulioanzia nchini Marekani kutokana na watu kushindwa kulipa mikopo ya nyumba, umeathiri uchumi wa dunia nzima.
Amesema mgogoro huo unaathiri misingi ya maisha ya watu wote. Ameeleza kuwa mgogoro huo ni Changamoto inayopaswa kukabiliwa na nchi zote duniani, kwa pamoja.
Akisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kuukabili mgogoro wa fedha ulioikumba dunia, naye rais wa tume ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barosso amezitaka nchi kutojaribu kukwepa changamoto inayotokana na mgogoro uliopo kwa kujitenga na kushughulikia mambo ya ndani kitaifa.
Amekumbusha kuwa nchi zote zimenufaika na biashara huru. Kwa hiyo lazima nchi zote ziepukane na tabia ya kujenga kuta ili kujitenga na wengine.
Akizungumza kwenye mkutano huo rais Nicolas Sarkozy wa Ufaranya ambae kwa sasa anauongoza Umoja wa Ulaya amezitaka nchi za Asia ziziunge mkono nchi za Ulaya kwenye mkutano muhimu juu ya uchumi utakaofanyika Washington mwezi ujao. ambapo viongozi kutoka nchi 20 , tajiri na zinazoinukia kiuchumi, pia watajadili njia za kuutatua mgogoro wa fedha.
Rais Sarkozy pia ametoa mwito wa kuleta mageuzi katika taratibu za shirika la fedha la kimataifa IMF na katika taasisi zingine zote zilizoundwa baada ya kumalizika vita kuu vya pili mwaka 1945.
Viongozi wa Ulaya na wa Asia wa jumuiya ya Asem kwenye mkutano wa Beijing wanatarijiwa kuwafiki wajibu wa shirika la IMF katika kuzisaidia nchi zilizoathirika kwa kiwango kikubwa na mgogoro wa fedha.