1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa viongozi wa Ulaya waingia siku ya pili

18 Julai 2020

Viongozi wa Umoja wa UIaya wanakutana kwa siku ya pili ya mazungumzo ya ana kwa ana kuhusu mpango mkubwa wa kichocheo ili kuupiga jeki uchumi ulioharibiwa na janga la virusi vya corona.

EU-Sondergipfel zur Bewältigung der Corona-Wirtschaftskrise
Picha: picture-alliance/dpa/EPA/S. Lecocq

Wengi wa viongozi wa nchi 27 wanachama walisema mara tu walipowasili kwa mkutano wao wa kwanza wa kilele wa ana kwa ana baada ya miezi mitano kuwa mpango huo ni muhimu kwa ajili ya kuuokoa uchumi ambao umeporomoka na kuongeza imani katika Umoja wa UIaya, ambao kwa miaka mingi umeyumba kutoka kwa mgogoro mmoja hadi mwingine.

Lakini maafisa wamesema kundi la mataifa tajiri ya kaskazini yakiongozwa na Uholanzi yanasisitiza msimamo wao kuhusu upatikanaji wa mfuko wa kuufufua uchumi, huku likipata upinzani kutoka Ujerumani, Ufaransa, mataifa ya kusini Italia na Uhispania na mataifa ya Ulaya mashariki.

Wajumbe wamesema viongozi hao 27 wanapingana kuhusu ukubwa wa jumla wa mpango huo, mgawanyiko kati ya ruzuku na mikopo inayoweza kulipwa katika mfuko wa kuufufua uchumi na masharti ya kisheria yanayoambatanishwa.

Ni mkutano wa kwanza wa ana kwa ana katika miezi mitanoPicha: Reuters/F. Lenoir

Lakini kikwazo kilikuwa kuhusu mchakato wa kutathmini namna ya kupata msaada, amesema afisa wa EU, wakati Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte akidai kuwa nchi moja huenda ikazuia malipo kutoka kwa mfuko huo kama mataifa wanachama yatarudi nyuma kuhusu mageuzi ya kiuchumi.

"Kama yanataka mikopo na hata misaada basi nadhani inaingia akili kuwa niwaeleze watu wa Uholanzi…kuwa nayo mageuzi hayo yawe yamefanyika." Alisema Rutte akikadiria kuwa nafasi za muafaka ni hamsini kwa hamsini.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ambaye aliadhimisha mwaka wake wa 66 wa kuzaliwa akiwa kwenye meza ya mazungumzo mjini Brussels, alikuwa muangalifu kuhusu nafasi za kufikia makubaliano, akitarajia "mazungumzo magumu kweli kweli".

Uchumi wa nchi za Umoja wa Ulaya upo katika mdororo mkubwa na wakati hatua za dharura za kuuokoa kama vile mipango ya kipindi kifupi ikielekea kuisha, hali inaonekana kuwa mbaya.

Umoja wa Ulaya tayari unakabiliana na sakata la Uingereza kujiondoa katika jumuiya hiyo na umeathirika na mizozo ya nyuma, kuanzia mporomoko wa kiuchumi wa 2008 hadi kwa ugomvi kuhusu uhamiaji.

Mgogoro mwingine wa kiuchumi huenda ukaiweka katika hali ngumu mbele ya wanaoeleza mashaka katika sera za Ulaya, wanaounga mkono siasa kali za kizalendo na wanaolinda masoko yao, na kudhoofisha nafasi yake dhidi ya China, Marekani au Urusi.

Reusters, AFP, DPA

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW