1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Viongozi wa Umoja wa Ulaya waanza Brussels

22 Machi 2018

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakabiliwa na ajenda iliyo na masuala chungu nzima wakati wakijitayarisha kujadili hatua ya Uingereza kujitoa katika Umoja huo katika mkutano wa siku mbili mjini Brussels.

Belgien EU Gipfel - Kurz, Tusk, Merkel
Picha: Reuters/W. Rattay

Viongozi wa mataifa hayo 27 yatakayobakia ndani ya Umoja wa Ulaya baada ya Uingereza kujitoa, wanatarajiwa kuidhinisha muongozo wa mazungumzo ya siku za usoni ya kuwa na mahusiano ya kibiashara na Uingereza, na kukubali mpango uliofikiwa wiki hii juu ya kipindi cha mpito.

Viongozi hao wanaokutana mjini Brussels pia wanatarajiwa kuyajibu masuala kadhaa ikiwemo shambulio la sumu dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi Sergei Skripal pamoja na mwanae wa kike, shambulio lililofanyika mjini Salisbury nchini Uingereza. 

Aidha Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May anatarajiwa kuwatolea mwito viongozi hao kuungana pamoja na kukikosia Urusi dhidi ya shambulio la Skripal. Uingereza ambayo imeinyooshea kidole cha lawama Urusi juu ya kisa hicho, imeitaja nchi hiyo kama kitisho katika mataifa ya Magharibi. Hata hivyo Urusi imeendelea kukanusha madai hayo.

Viwango vipya vya ushuru kwa bidhaa za chuma na bati kujadiliwa kwa kina

Picha: Reuters/W. Rattay

Kando na hilo suala jengine linalopewa kipaumbele katika ajenda ya mazungumzo ya mkutano huu ni lile la Marekani kupitisha viwango vipya vya juu vya ushuru kwa bidhaa kutoka nje za chuma na bati hatua inayotazamiwa kuanza rasmi mwishoni mwa wiki hii. Umoja wa Ulaya hautaki kuwepo katika nchi zinazotozwa ushuru huo.

Kwa upande wake naibu rais wa halmashauri ya Umoja huo Jyrki Katainen amesema huenda wakafikiria hatua nyengine za kuchukua iwapo rais wa Marekani Donald Trump hatowaacha nyuma katika ongezeko hilo la ushuru.

Marekani inatarajiwa kuanza kutoza ushuru wa bidhaa za bati na chuma zinazoingizwa nchini mwake, asilimia 25 kwa chuma na asilimia 10 kwa bati,Canada na Mexico nchio nchi pekee zilizotangazwa rasmi kutolipa ongezeko hilo.

Wakati huo huo uhusiano wa Umoja wa Ulaya na Uturuki pia utajadiliwa kwa kina wakati maafisa wakuu wa Umoja wa Ulaya wakijitayarisha kukutana na rais Recep Tayyip Erdogan  mjini Varna Bulgaria siku ya Jumatatu. Umoja wa Ulaya pia utaikosoa vikali Uturuki kwa kuzuwiya uchimbaji wa mafuta na gesi katika pwani ya Cyprus, badala yake umeitaka Uturuki kuheshimu haki ya watu wa Cyprus ya uchimbaji wa mali asilia.

Kisiwa cha Cyprus kimegawika tangu mwaka 1974 upande mmoja ukiwa  Kusini mwa Ugiriki ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya na na upande mwengine Kaskazini mwa Uturuki inayotambulika na Uturuki pekee.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/AFP/ Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW