1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya

30 Oktoba 2009

Viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels wamepata makubaliano yanayofungua njia ya kuidhinisha Mkataba wa Lisbon, lakini hawakuweza kukubaliana kuhusu gharama za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani.

European Commission President, Jose Manuel Barroso addresses reporters during a news conference after his reelection at the European Parliament in Strasbourg, eastern France, Wednesday, Sept. 16, 2009. The European Parliament gave Barroso another five-year term as European Commission president Wednesday, but its vote reflected lingering misgivings about the conservative ex-Portuguese premier in the EU assembly. (AP Photo/Christian Lutz)
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya,Jose Manuel Barroso.Picha: AP

Inaonekana Mkataba wa Lisbon unakaribia kuidhinishwa.Kwani jana baada ya kumalizika majadiliano ya siku ya kwanza ya mkutano huo wa siku mbili mjini Brussels, Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso, kwa furaha alieleza hivi:

"Makubaliano yaliyopatikana leo usiku ni muhimu kabisa. Mnajua, mkataba mpya unanikumbusha mbio za masafa marefu, lakini za kuruka viunzi. Ninaamini kuwa tumeondosha kikwazo cha mwisho cha kisiasa kwa hivyo,hivi karibuni Mkataba wa Lisbon utaweza kuanza kutumika."

Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wamekubali sharti la Jamhuri ya Czeki kutofungamanishwa na Mkataba wa Haki za Msingi. Hivi karibuni Rais wa nchi hiyo, Vaclav Klaus, alisema hilo ni sharti la nchi yake kuidhinisha Mkataba wa Lisbon. Kwa njia hiyo, anataka kuhakikisha kuwa Wajerumani waliofukuzwa kutoka Czechoslovakia ya zamani baada ya Vita Vikuu vya Pili, hawatoweza kudai mali yao kuambatana na Mkataba wa Haki za Msingi. Kwa hivyo,mahakama ya katiba ya Jamhuri ya Czeki ikitupilia mbali mashtaka yaliyotolewa na wabunge wa kihafidhina wa nchi hiyo kupinga Mkataba wa Umoja wa Ulaya uliofanyiwa marekebisho basi mkataba huo utaweza kuanza kutumika mwisho wa mwaka huu.

Kwa upande mwingine, suala la ulinzi wa mazingira limezusha mabishano makali kati ya viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels. Mvutano huo hasa unahusika na gharama za kuzisaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na njia ya kugawana mzigo huo katika Umoja wa Ulaya. Nchi wanachama 27 katika umoja huo zimetazamia kuwa na msimamo mmoja kuhusu mada hiyo, kabla ya kwenda kwenye mkutano wa kimataifa wa mazingira, utakaofanywa mwezi wa Desemba katika mji mkuu wa Denmark Copenhagen. Lakini wanachama wengi kutoka Ulaya ya Mashariki wana hofu kuwa gharama hizo zitakuwa kubwa sana.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.Picha: AP

Kwa upande mwingine,Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesisitiza dhima ya Ulaya inayoshika bendera katika ulinzi wa mazingira.Amesema:

"Sisi huku tutaeleza wazi kabisa fikra zetu. Vile vile tutaeleza wazi wazi kwamba tupo tayari kuchukua hatua ya mwanzo na kuwajibika na bila shaka baadae kuonyesha mfano kwa kutoa msaada wa fedha."

Kwa maoni ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, kiasi cha Euro bilioni 100 zitahitajiwa hadi mwaka 2020. Na sehemu kubwa ya pesa hizo zitalipwa na nchi za barani Ulaya. Iwapo mwito huo utaitikiwa na wanachama wenzake itajulikana baadae leo hii mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya utakapomalizika. Kwani Brown aliempendekeza Tony Blair kuchaguliwa kuwa rais wa Baraza la Ulaya, hakuungwa mkono na viongozi wengi wa Umoja wa Ulaya. Huo ni wadhifa mpya ulioundwa kuambatana na Mkataba wa Lisbon. Wadhifa mwingine mpya wa pili wa ngazi ya juu katika Umoja wa Ulaya ni wa Waziri wa Mambo ya Nje.

Mwandishi:S.Henn /ZPR /P.Martin

Mhariri: Othman, Miraji

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW