1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa viongozi wakuu wa Ufaransa na Afrika wamalizika .

Mohammed AbdulRahman5 Desemba 2005

Watahadharisha juu ya mwenendo wa biashara huru.

Rais wa Mali Ahmadou Toumani Toure, aliyekua mwenyeji wa mkutano huo.
Rais wa Mali Ahmadou Toumani Toure, aliyekua mwenyeji wa mkutano huo.Picha: AP

Mkutano wa 23 wa viongozi wakuu wa Ufaransa na Afrika umemalizika katika mji mkuu wa Mali-Bamako,huku Rais wa Ufaransa Jacques Chirac na viongozi wa nchi za kiafrika wakionya juu ya mwenendo wa uhuru wa kibiashara katika biashara ya kimataifa, jambo ambalo linaweza kuziathiri nchi masikini.

Rais Chirac alikua akizungumza katika mkutano na waandishi habari, mwishoni mwa mkutano mkuu wa viongozi kati ya Ufaransa na nchi za kiafrika hapo jana. Viongozi wa kiafrika waliohudhuria mkutano huo wa siku mbili katika mji mkuu wa Mali-Bamako ni pamoja na Rais mteule wa Liberia Bibi Ellen Johnson Sirleaf,Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Thabo Mbeki wa Afrika kusini na Omar Bongo wa Gabon ambaye ndiye kiongozi aliyeko madarakani kwa muda mrefu kabisa barani Afrika akiwa anatawala kwa mwaka wa 38 sasa.

Kiongozi wa Ivory Coast Laurent Gbagbo hakuhudhuria.

Rais Chirac alisema kwa pamoja wanaonya juu ya kile kinachoonekana kuwa ni mkondo wa biashara huru, jambo ambalo linaweza kuzusha athari kubwa kwa mataifa ya kiafrika, kwani hali hiyo itaziridhisha zaidi nchi tajiri na zile zinazoinukia katika masuala ya biashara na kilimo ,na kuziathiri nchi masikini.

Akaongeza kwamba ukuaji uchumi wa asili mia 5 ni mzuri lakini hautoshi katika kupambana na umasikini.

Kwa upande mwengine ukatolewa wito wa kuzitaka nchi masikini kuongeza maradufu msaada wao wa maendeleo, huku viongozi hao wakionya kwamba ni muhimu kulishughulikia ipasavyo saula la kupambana na umasikini, ili kuzuwia wimbi la wahamiaji wasio halali wanaolihama bara hilo.

Maelfu ya watu wengi wao kutoka Afrika magharibi, mara nyingi kujaribu kuvuka jangwa la sahara katika mazingira magumu, na kujaribu kuingia Uhispania na baadae nchi nyengine za ulaya.wakilikimbia janga la umasikini mkubwa katika nchi zao.

Njia za kupambana na tatizo hilo, ni moja wapo ya masuala makuu yalioajadiliwa na Viongozi hao, ambao walisema linaweza kuatatuliwa kwa nchi za viwanda kuongeza msaada wao kwa nchi masikini, na utaratibu mpya kuhusu madeni.

Msimamo wa Bw Chirac , ulipongezwa na Rais wa Mali Amadou Toumani Toure aliyekua mwenyeji wa mkutano huo, akisema kiongozio huyo wa Ufaransa ana hisia na Afrika.

Mkutano wa Bamako umefanyika wakati juhudi za kimataifa zikiendelea, kuunusuru mkutano wa mawaziri wa shirika la biashara duniani WTO, utakaofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 18 ya mwezi huu mjini Hong kong, ukiwa na lengo la kufikiwa mkataba juu ya uhuru wa biashara duniani , uweze kuanza kufanya kazi mwaka ujao.

Hadi sasa duru nne za mazungumzo zimekwama, kuhusiana na kiwango cha fedha ambacho nchi tajiri hutoa kama msaada wa kufidia sekta zao za kilimo nyumbani. Ufaransa ndiyo inayofaidika zaidi na fidia katika sekta hiyo kutoka Umoja wa ulaya.

Wakati Halmashauri kuu ya ulaya imesema itapigania uachwe mtindo wa kufidia sekta ya kilimo cha pamba, Rais Chirac aliitaka Marekani kuondoa mtindo wa kufidia wakulima wake.

Suala jengine muhimu lililojadiliwa ni vita dhidi ya janga la Ukimwi, na mgogoro wa Ivory Coast.

Mkutano wa kwanza Viongozi wakuu baina ya Ufaransa na Afrika uliitishwa 1973 na sasa hufanyika kila baada ya miaka miwili kwa mtindo wa kupokezana kati ya Ufaransa na bara hilo.