1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaUlaya

Mkutano wa Gdańsk wajadili ujenzi mpya wa Ukraine

Zainab Aziz DPA/AFP/RTRE
25 Juni 2026

Mawaziri wakuu wa Poland Donald Tusk na wa Ukraine Yulia Svyrydenko, wameufungua Mkutano wa Ujenzi mpya wa Ukraine katika mji wa pwani wa Gdańsk ulio kaskazini mwa Poland.

Polen Danzig 2026 | Ukraine Recovery Conference | Tusk & Swyrydenko beim Familienfoto
Mkutano wa wafadhili wa Gdańsk kujadili ujenzi mpya wa UkrainePicha: Lukasz Glowala/REUTERS

Mkutano huo wa siku mbili, ulioandaliwa kwa pamoja na Poland na Ukraine, umewaleta pamoja viongozi na wakuu wa taasisi za fedha za kimataifa kujadili msaada wa kiuchumi kwa Ukraine.

Rais Voldymyr Zelensky hahudhurii mkutano huu muhimu kuhusu ujenzi mpya wa Ukraine baada ya vita, kutokana na ugomvi wa kidiplomasia kati ya Ukraine na mshirika wake Poland uliosababishwa na Ukraine ilipokipa kikosi chake cha kijeshi jina la kundi moja la waasi lililoshiriki katika mauaji ya Wapoland wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Hata hivyo Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk na mwenzake wa Ukraine Yulia Svydyrenko, walipofungua Mkutano huo wa kila mwaka waliituliza hali hiyo ya mvutano wa kidiplomasia kati ya nchi zao mbili.

Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk Picha: Yiannis Kourtoglou/REUTERS

Mkutano huo unalenga kuimarisha misaada ya kimataifa kwa ajili ya ujenzi mpya wa Ukraine na pia kuchochea uwekezaji kwenye biashara za nchini humo.

Sekta za nishati na miundombinu kupewa kipaumbele

Mkazo ukitiliwa zaidi katika sekta zilizoathiriwa zaidi na vita vya Urusi, ikiwa ni pamoja na sekta za nishati na miundombinu muhimu.

Katika hotuba ya ufunguzi Waziri Mkuu wa Ukraine Yulia Svydyrenko, alisema:

"Katika siku mbili zijazo za mkutano huu, tunatarajia kutia saini mikataba zaidi ya 160 ambayo ina thamani ya zaidi ya euro bilioni 10. Mikataba hiyo inalenga kukusanya rasilimali na uwezo katika nyanja kuu tano: Kujumuishwa kwenye Umoja wa Ulaya, rasilimali watu, biashara, maendeleo ya ndani na ya kikanda na kwa mara ya kwanza katika mwaka huu hapa Gdansk, tunao mwelekeo unaozingatia ulinzi."

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk Picha: Adam Warzawa/PAP/dpa/picture alliance

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema sehemu ya kwanza ya euro bilioni 3.2 ya mkopo wa Euro bilioni 90 kutoka Umoja wa Ulaya imetolewa leo Alhamisi na Wizara ya Fedha ya Ukraine imethibitisha kupokea kitita hicho.

Ukraine imesema itatumia mkopo huo kwa ajili ya ulinzi na usalama, nishati na kuziba pengo kwenye nakisi ya bajeti yake.

Von der Leyen amesema mfuko wa uwekezaji ulioahidiwa kwa ajili ya ujenzi mpya wa Ukraine, unaoungwa mkono na Umoja wa Ulaya, Ufaransa, Ujerumani na Poland, pia umejiandaa kukusanya takriban euro milioni 500 mwaka huu.

Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk ametoa wito kwa nchi za Magharibi kuamini kwamba Ukraine "itainuka kutoka kwenye magofu" baada ya vita kama ulivyo mji wake wa Poland, Gdansk, ulioharibiwa kwa kiasi kikubwa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW