1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wamalizika bila ya mafanikio thabiti

14 Desemba 2017

Mawaziri wa biashara kutoka nchi 164 wanachama wa WTO katika mkutano huo wa siku tatu walijadili masuala ya biashara yaliyohusisha chakula, kilimo, biashara, maendeleo na ruzuku kwa ajili ya uvuvi.

Argentinien WTO Konferenz in Buenos Aires
Picha: picture alliance/dpa/AP Photo/N. Pisarenko

Mkwamo uliotokea kwenye mkutano huo uliondoa matumaini ya kufikiwa mikataba mipya ya biashara kwa lengo la kukomesha ruzuku zinazotolewa katika sekta za kilimo na uvuvi. Mkwamo huo pia umezua maswali mengi iwapo shirika hilo lina uwezo wa kuongoza katika dunia inayozidi kutingwa na mizozo ya kibiashara.

Hali ya kukatisha tamaa iliwafanya baadhi ya wajumbe kama vile mwakilishi wa Marekani Robert Lighthizer, ashauri kuwa ni bora mazungumzo yafanyike miongoni makundi madogo madogo ya wajumbe kutoka nchi zenye mitazamo inayofanana.

Mkurugenzi mkuu wa WTO Roberto AvezedoPicha: picture alliance/dpa/AP Photo/N. Pisarenko

Akiufunga mkutano huo mkurugenzi mkuu wa WTO Roberto Azevédo amesema amesikitika kwamba wajumbe hawakuweza kufikia makubaliano. Mkurugenzi huyo mkuu wa WTO ameongeza kusema wanachama wa shirika hilo wanapaswa kujitathmini namna ya kusonga mbele na watambue kwamba haiwezekani kupata kila kitu wanachotaka. Ameeleza kwamba wanachama wanahitaji kupiga hatua ndefu katika mitazamo yao.

Kwa upande wake kamishna wa biashara wa Umoja wa Ulaya Cecilia Malmström amewaambia waandishi wa habari kuwa amesikitishwa na ukweli kwamba safari hii hawakuweza hata kufikia makubaliano juu ya kusitisha kutolewa ruzuku kwa ajili ya uvuvi haramu. Bibi Malmström amesema mkutano huo umeonyesha moja kati ya mapungufu makubwa ya shirika hilo la biashara duniani WTO ambalo wakati wote linahitaji wanachama wake wote164 waseme kwa kauli moja ili makubaliano yapitishwe, na amesema Marekani inabeba sehemu ya lawama lakini nchi nyingine pia zilizuia hatua za kusonga mbele.

Mjumbe wa Marekani katika mkutano wa WTO Robert LighthizerPicha: Getty Images/E.Abramovich

Mkutano wa mjini Buenos Aires ulianza vibaya baada ya mjumbe wa Marekani kusema kwamba shirika hilo la WTO linapoteza lengo lake kuhusu mazungumzo ya biashara na badalayake linageuka kuwa shirika kushtakiana. Mjumbe huyo amesema baadhi ya wanachama wa WTO wanajaribu kujinufaisha kwa njia ya kupeleka kesi mahakamani manufaa ambayo hawawezi kuyapata kwenye meza ya mazungumzo.

Marekani kwa muda mrefu imekuwa mtetezi wa shirika hilo la biashara duniani WTO lakini rais Donald Trump amesema kwamba nchi yake haitendewi haki na shirika hilo na amepunguza ushiriki wa Marekani wa kuliongoza shirika hilo.

Kushindwa kwa wajumbe kukubaliana juu ya mikataba mipya ina maana kwamba mada hiyo ya biashara itaendelea kubakia kama ilivyo. Wajumbe wa WTO hata hivyo wamekubaliana kuweka jitihada katika kulifikia lengo jipya kuhusu ruzuku ya uvuvi katika mkutano mwingine wa mawaziri utakaofanyika mwaka wa 2019.

Mwandishi:Zainab Aziz/RTRE/APE

Mhariri: Caro Robi

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW