Mkuu mpya wa jeshi ateuliwa Armenia
10 Machi 2021Agizo la Pashinyan limeanza kutumika hii leo, baada ya kumtimua mkuu wa jeshi Onik Gasparyan kwa tuhuma za kupanga njama ya mapinduzi baada ya mkuu huyo wa jeshi kutoa mwito wa kutaka Panshinyan ajiuzulu.
Waziri mkuu huyo wa Armenia amekuwa akikabiliwa na shinikizo la kutakiwa kujiuzulu kutokana na jinsi alivyoshughulikia mzozo kati ya nchi yake na Azerbaijan kuhusu mkoa wa Nagorno Karabakh. Soma zaidi Mvutano wa kisiasa wapamba moto Armenia
Mwito wa Gasparyan mnamo februari 25 wa kutaka Pashinyan ajiuzulu uliibua maandamano makubwa katika mji mkuu wa Yerevan sio tu kutoka kwa wakosoaji wa waziri mkuu huyo bali pia kwa wale wanao muunga mkono.
Leo hii waziri mkuu Pashinyan amesema agizo lake litaanza kuheshimiwa. Msemaji wa serikali Nune Gevorgyan ameliambia shirika la habari la AFP kuwa Waziri mkuu huyo ametoa wito kwa rais Armen Sarkisian kumteua Generali Luteni Artak Davtyan kama mkuu wa jeshi.
Gasparyan akubali kutimuliwa
Hata hivyo Gasparyan amekubali kutimuliwa kwake bila kusita, na akasema kuwa ili kudhihirisha mamlaka ya kikatiba na sheria ya Armenia na atakata rufaa dhidi ya amri ya waziri mkuu.
Taarifa kutoka kwa Ofisi ya rais Armen Sarkissian imedokeza kuwa rais huyo ameiomba mahakama ya kikatiba kutazama uhalali wa kutimuliwa kwa jenerali Gasparyan.
Shirika la habari la TASS limeripoti kuwa viongozi wa jeshi la Armenia pia walisisitiza wito wao wa kumtaka Waziri Mkuu Nikol Pashinyan ajiuzulu licha ya tangazo rasmi la kumfuta kazi aliyekuwa mkuu wao.
Maandamano Yerevan
Mara kwa mara waandamanaji wameingia mitaani mjini Yerevan kudai kujiuzulu kwa waziri mkuu Pashinyan tangu aliposaini makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Urusi na Azabaijan mnamo Novemba ambayo yalimaliza wiki sita za mzozo juu ya jimbo la Nagorno-Karabakh.
Chini ya makubaliano hayo ambao wengi nchini Armenia wanauona kama udhalilishaji wa kitaifa, Armenia ilikubali kuachia baadhi ya maeneo kwa Nagorno Karabakh na kuyakabidhi kwa Azerbaijan.
Pashinyan, ambaye amekataa wito wa kujiuzulu, amesema alilazimika kukubali mkataba wa amani ili kuzuia hasara kubwa za kibinadamu na za kitaifa. Soma zaidi Makubaliano mapya yatangazwa Nagorno-Karabakh
Waziri mkuu huyo amekuwa madarakani tangu mwaka 2018 katika nchi hiyo ambayo zamani ilikuwa sehemu ya iliyokuwa Umoja wa Kisovieti.