1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo Gaza vafikia 36,555, Ukingo wa Magharibi kwafukuta

4 Juni 2024

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk amesema Jumanne kuwa kanuni na viwango vya uendeshaji wa vita vimekiukwa kikatili huko Gaza, na kutangaza kuunga mkono mpango wa Marekani wa kukomesha vita hivyo.

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk
Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker TurkPicha: KHALED DESOUKI/AFP

Mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ametaka kukomeshwa kwa ghasia zinazoendelea katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, akisema ni jambo lisiloeleweka kwamba zaidi ya Wapalestina 500 wameuawa huko tangu Oktoba 7.

Volker Turk alisema takriban Wapalestina 505 wameuawa katika Ukingo wa Magharibi na jeshi la Israel na walowezi wa Ukingo wa Magharibi tangu kuzuka kwa vita vya Gaza karibu miezi minane iliyopita. Maafisa wa Palestina wametoa idadi ya watu wasiopungua 523.

Soma pia: Zaidi ya nusu ya miundombinu yote Ukanda wa Gaza imeharibiwa

Dazeni mbili za Waisraeli, wakiwemo wanajeshi wanane, pia wameuawa katika mapigano ya Ukingo wa Magharibi au mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na Wapalestina kutoka Ukingo wa Magharibi katika kipindi hicho, alisema.

Mashambulizi ya Israel Gaza yameacha sehemu kubwa ya Ukanda huo ikiwa magofu, huku watu zaidi ya elfu 36 wakiuawa, wengi wao wanawake na watoto.Picha: Mahmoud Zaki/Xinhua/picture alliance

"Kana kwamba matukio ya kutisha nchini Israel na Gaza katika kipindi cha miezi minane iliyopita hayatoshi, watu wa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu pia wanakabiliwa na umwagaji wa damu usio na kifani siku baada ya siku," alisema Volker Turk katika taarifa yake.

"Haifikiriki kwamba maisha ya watu wengi yameangamizwa kwa mtindo huo wa kitovu."

Turk alisisitiza "mauaji, uharibifu na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu haukubaliki, na lazima ukomeshwe mara moja".

"Israeli lazima sio tu idhinishe, lakini pia itekeleze sheria za vita ambazo zinaendana kikamilifu na kanuni na viwango vinavyotumika vya haki za binadamu," alisema, akitaka uwajibikaji kwa madai yote ya mauaji kinyume cha sheria.

Turk ameshutumu hali ya "kutokuadhibiwa kwa uhalifu kama huo" katika Ukingo wa Magharibi, ambao Israeli imeukalia tangu 1967, na ambao umeshuhudia kuongezeka kwa ghasia hata kabla ya Oktoba 7.

Alitaja kisa cha mwishoni mwa wiki ambapo vikosi vya Israel vilimpiga risasi na kumuua kijana mmoja na kumjeruhi vibaya mwingine ambaye baadaye alifariki karibu na kambi ya wakimbizi ya Aqabat Jabr karibu na Yeriko katika Ukingo wa Magharibi.

Soma pia:Israel yakanusha madai kuhusu makaburi ya pamoja Gaza

Alisema picha za CCTV zilionyesha kuwa wavulana hao walipigwa risasi kwa umbali wa mita 70 walipokuwa wakikimbia baada ya kurusha mawe na/au vilipuzi vya kutengenezwa kienyeji kuelekea kituo cha kijeshi.

Watoto wa Gaza wakichezea glavu za hospitali walizozigeuza baluni.Picha: Eyad Baba/AFP

Taarifa ya Turk ilisema jeshi la Israel mara nyingi limekuwa likitumia nguvu za mauaji "kama suluhu ya kwanza dhidi ya waandamanaji wa Kipalestina ... katika hali ambapo wale waliopigwa risasi hawakuwakilisha tishio la maisha."

Turk alionya kwamba ghasia "kwa msingi wa ukubwa wa mauaji na uharibifu unaoendelea Gaza, zimezua hofu na ukosefu wa usalama miongoni mwa Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu".

Wizara ya afya Gaza: Vifo katika vita vyafikia 36,550

Mamlaka ya afya katika Ukanda wa Gaza imeripoti kuwa idadi ya Wapalestina waliouawa katika vita vinavyoendelea huko imepanda hadi 36,550.

Katika muda wa saa 24, jeshi la Israel limeua Wapalestina 40 na kuwajeruhi wengine 150, na kufikisha jumla ya waliojeruhiwa- kuwa elfu 82 na 777 tangu kuzuka kwa mzozo wa kivita kati ya Israel na Wapalestina Oktoba 2023.

Soma piaWatu 104 wauwawa katika operesheni ya kutoa msaada Gaza

Vikosi vya jeshi la Israel, IDF, vilisema Jumatatu kuwa vimeendeleza operesheni kote katika Ukanda wa Gaza.

Shirika rasmi la habari la Palestina, WAFA, limeripoti kuwa jeshi la Israel lililifanya mashambulizi makubwa ya mabomu kote Gaza siku hiyo ya Jumatatu, na kusababisha vifo vingi, huku makundi ya wapiganaji wa Kipalestina yakidai pia kuyashambulia maeneo ya Israel Gaza.

Imamu na Rabbai waunganisha jamii katikati ya mzozo wa Gaza

03:11

This browser does not support the video element.

Katika taarifa yake ya Jumatatu, jeshi la Israel lilisema ndege zake za kivita zilishambulia zaidi ya maeneo 50 ya Wapalestina, ikiwemo maghala ya silaha.

Katika eneo la Rafah kusini mwa Gaza, jeshi la Israel liliendelea kufanya kile lilichokiita operesheni makhsusi, na katikati mwa Gaza, jeshi hilo liliuwa Wapalestina wengi na wapiganaji.

WAFA pia iliripoti Jumatatu kwamba katika siku iliyopita, jeshi la Israeli lilifanya mashambulizi mengi ya anga kwenye mji wa Gaza kaskazini mwa ukanda huo, kambi za wakimbizi za Bureij na Nuseirat katikati mwa Gaza, na mji wa kusini wa Khan Yunis, na kusababisha vifo vingi.

Israel pia imeendeleza operesheni zake katika eneo la Ukingo wa Magharibi ambapo mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk, amesema Wapalestina zaidi ya 500 wameuawa huko tangu Oktoba 7, na kutaka kukomeshwa kwa mauaji hayo.

Marekani yatafuta uungwaji mkono wa Baraza la Usalama

Marekani imelihimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo Jumatatu kuunga mkono mpango wa awamu tatu uliotangazwa na Rais Joe Biden unaokusudiwa kukomesha vita hivyo vilivyodumu kwa takribani miezi nane.

Balozi wa Marekani Linda Thomas-Greenfield alisema Marekani ilisambaza rasimu ya azimio kwa wajumbe wengine 14 wa baraza kuunga mkono pendekezo la kumaliza mzozo ulioanza na shambulio la kushtukiza la Hamas kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7 na kuua takriban watu 1,200, wengi wao wakiwa raia.

Mapacha vichanga wauwawa Gaza

01:04

This browser does not support the video element.

"Viongozi wengi na serikali, ikiwa ni pamoja na katika kanda, wameidhinisha mpango huu na tunatoa wito kwa Baraza la Usalama kuungana nao katika kutoa wito wa utekelezaji wa mpango huu bila kuchelewa na bila masharti zaidi," alisema katika taarifa yake.

Soma pia: Guterres asikitishwa na kuanza upya kwa vita Ukanda wa Gaza

Azimio hilo linakaribisha mpango wa Mei 31 uliotangazwa na Biden, na linatoa wito kwa Hamas kukubali kikamilifu na kutekeleza masharti yake bila kuchelewa na bila masharti. Hamas ilisema ina mtazamo chanya kuhusu mpango huo, ambao hata hivyo hautaji chochote kuhusu kukubaliana kwa Israel na mpango huo.

Mji wa Nagasaki wasitisha mwaliko kwa Israel

Katika hatua nyingine, mji wa Nagasaki ulioko kusini mwa Japan, umektaa kumualika Balozi wa Israel kuhudhuria sherehe yake ya kila mwaka ya amani, na badala yake ulituma barua ubalozi ukitoa wito wa usitishaji vita Gaza.

Mji huo umetuma mialiko wiki hii kwa mataifa kadhaa na maeneo kushirikia tukio hilo la Agosti 9, kukumbuka shambulio la nyuklia la Marekani mwaka 1945 lililouwa watu elfu 74.

Lakini "kuhusu Israel, hali inabadilika siku baada ya siku... kwa hivyo tumesimamisha kutuma barua ya mwaliko," meya Shiro Suzuki aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumatatu.

Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Ukanda wa Gaza

02:51

This browser does not support the video element.

Wasiwasi kwamba maandamano yanaweza kuvuruga kumbukumbu ya waathirika wa bomu la atomiki ni sababu mojawapo ya uamuzi huo, alisema Suzuki.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW