1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

China yasema siasa zisihusishwe na haki za binadamu

24 Mei 2022

Mashirika ya haki za binadamu yakhofia ziara ya Bachelet haitoleta mabadiliko yoyote ndani ya China

UN I Michelle Bachelet
Picha: Denis Balibouse/REUTERS

Mkuu wa haki za binadamu wa kamisheni ya Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet  yuko ziarani China ambako alikutana na waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi siku ya kwanza ya ziara yake hiyo hapo jana Jumatatu.

Ziara ya mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa,nchini China ni ya siku sita ikiwa na lengo la kutafuta ukweli kuhusu madai ya unyanyasaji na mateso dhidi ya jamii ya wachache ya Waislamu wa kabila la Uighuru katika jimbo la Xinjiang lililoko  KaskaziniMagharibi mwa China.

Hata hivyo mashirika ya haki za binadamu yanahofia kwamba ziara hiyo itasaidia kuyafunika matukio ya unyanyasaji ya maafisa wa China.

Picha: Sam McNeil/AP Photo/picture alliance

Tayari waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Wang Yi ambae alikutana na Bachelet katika mji wa kusini mwa China wa Guangzhou  ameshamwambia mkuu huyo wa haki za binadamu kwamba China  haiungi mkono suala la kuhusisa haki za binadamu na siasa,kadhalika haikubaliani na undumilakuwili.

Kwa upande wake mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amebaini yuko tayari kuwa na mazungumzo yenye tija na maafisa wa China.

"Tutakapojadiliana baadhi ya masuala muhimu zaidi na nyeti nataraji itatusaidia kujenga imani na kutuwezesha kufanya kazi pamoja kuendeleza uungaji mkono na ushirikiano katika suala la haki za binamau ndani ya China lakini pia katika ngazi ya ulimwengu.''

Umoja wa Mataifa umesema Bachelet alitarajiwa kuzungumza na watu mbali mbali wakati wa ziara yake hiyo na hasa maafisa wa serikali,viongozi wa kibiashara,wasomi,wanafunzi pamoja na wanachama wa mashirika ya kiraia wanaoshughulikia haki za binadamu  na masuala mengine ya kijamii na kiuchumi.

China imewafungia watu wa jamii ya Uighur, Kazakh na jamii nyingine za wachache za waislamu  kiasi milioni moja au zaidi  katika kile ambacho wakosoaji wanakiita ni kampieni ya kuwalazimisha kuachana na tamaduni zao zinazowatambulisha.

Picha: Salvatore Di Nolfi/KEYSTONE/picture alliance

Lakini kwa upande wake serikali ya China inasema haina cha kukificha na inawakaribisha watu wote wasiokuwa na mitizamo ya kisiasa ya kuibagua nchi hiyo kuitembelea Xinjiang na kujionea kile inachokiita kampeini ya mafanikio ya kupambana na ugaidi  na kurudisha utulivu na mjongeleano wa kimadhehebu.

Bachelet anakwenda Kashgar baada ya kuondoka Guangzhou na huko atautembelea mji mkuu wa jimbo la Xinjiang,Urumqi. Umoja wa Mataifa na China wamezuia vyombo vya habari vya kigeni kuandamana na Bachelet na haijulikani hasa atakutana na nani na kuruhusiwa kuyatembelea maeneo gani katika ziara yake nzima.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW