1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa IAEA aridhishwa mazungumzo na Iran

4 Machi 2023

Mkuu wa shirika la kimataifa la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia amesema mazungumzo yake na maafisa wa Iran yamekuwa ya manufaa makubwa, huku Iran ikiyataka mataifa makubwa kutimiza wajib wao Mkataba wa Nyuklia.

Iran | IAEA Generaldirektor Rafael Mariano Grossi in Teheran
Picha: Vahid Salemi/AP Photo/picture alliance

Ziara hiyo ya siku mbili ya mkuu huyo wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), Rafel Grossi, ilifanyika wakati shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Vienna likitaka pawepo ushirikiano mkubwa zaidi na Tehran juu ya shughuli zake za kinyuklia.

"Kwa kuwa na majadiliano madhubuti na makubaliano mazuri, kama ambayo nina hakika tutakuwa nayo, tutasafisha njia kuelekea makubaliano muhimu," Grossi aliwaambia waandishi wa habari mjini Tehran akiwa na mwenyeji wake, mkuu wa programu ya nyuklia ya Iran, Mohammad Eslami, siku ya Jumamosi (Machi 4).

Soma zaidi: IAEA kufunga Kamera mpya kwenye kituo cha nyuklia cha Iran
Mazungumzo ya kufufua mkataba wa nyuklia wa Iran kuanza tena

Kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, Eslami alitoa wito kwa mataifa yaliyosaini Mkataba wa Nyuklia wa 2015, maarufu kama JCPOA, kutimiza wajibu wao.

Mkuu wa Shirika la Nguvu ya Atomiki duniani, Rafael Grossi (kushoto), akizungumza na Waziri wa Mambo ya Kigeni ya Iran, Hossein Amir Abdollahian, mjini Tehran.Picha: dpa/XinHua/picture alliance

"Nchi tatu za Ulaya na baadhi ya nchi nyengine zinajikita tu kwenye wajibu wa Iran kwenye JCPOA. Nazo pia zina wajibu wanaopaswa kuutekeleza. Tumekubaliana (na Grossi) kufafanua ushirikiano wetu ndani ya mfumo wa usalama," alisema Eslami.

Grossi aliwasili Iran siku ya Ijumaa (Februari 3) huku kukiwa na mkwamo kwenye majadiliano ya kuufufua Mkataba wa JCPOA.  

Kuelekea mwanzo mpya

Mkuu huyo wa IAEA alikutana na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian, siku ya Jumamosi na baadaye alitazamiwa pia kukutana na Rais Ebrahimi Raisi kwenye ziara yake ya "kuzinduwa tena majadiliano" juu ya shughuli za atomiki za Iran na "kuunda upya mahusiano ya ngazi za juu."

Picha: Dado Ruvic/REUTERS

Mkuu huyo wa IAEA alikuwa ameweka bayana kwamba "angelikwenda Tehran tu baada ya kupokea mwaliko wa kuzungumza na Rais Raisi," kwa mujibu wa chanzo hicho.

Soma zaidi: IAEA: Iran inaongeza akiba yake ya madini ya urani
Iran kuanza tena mazungumzo ya nyuklia
Shirika la IAEA laikosoa Iran kwa kukwamisha kazi yake

 

Chembechembe zilizorutubishwa kwa kiwango asilimia 83.7 - chini kidogo ya asilimia 90 zinazohitajika kutengeneza bomu la nyuklia - ziligunduliwa wiki hii kwenye chumba cha chini cha kinu cha Fordow kilicho umbali wa kilomita 100 kusini mwa mji mkuu wa Iran, Tehran, kwa mujibu wa ripoti ya siri ya IAEA iliyolifikia shirika la habari la AFP.

Tehran inakanusha shutuma kwamba inataka kuwa na silaha za nyuklia na ilikuwa inashikilia haijawahi kurutubisha madini ya urani juu ya kiwango cha asilimia 60, na sasa inadai kuwa "huenda kulitokea makosa wakati wa mchakato wa urutubishaji."

Ugunduzi huo ulifanyika baada ya Iran wakati Iran ikifanya marekebisho kwenye kinu chake bila ya kuieleza IAEA.

Vyanzo: AFP, dpa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW