1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Mkuu wa IAEA azuru Kinu cha nyuklia cha Kursk nchini Urusi

27 Agosti 2024

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti matumizi ya nishati ya Atomiki – IAEA Rafael Grossi ameanza leo ziara ya kufanya uchunguzi huru wa hali ilivyo katika kinu cha nyuklia cha Kursk nchini Urusi.

Kinu cha nyuklia cha Kursk
Vikosi vya Ukraine na Urusi vinapambana katika eneo la Kursk karibu na kinu cha nyukliaPicha: Vladimir Gerdo/TASS/dpa/picture alliance

Msemaji wa shirika la nyuklia la Urusi, Rosatom, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa Rossi aliwasili katika kinu cha Kursk wakati akiongoza ujumbe wa kutathmini hali ilivyo, ambayo ameonya kuwa ni "mbaya mno".

Grossi, alioneshwa kwenye televisheni ya taifa ya Urusi akizungumza na maafisa wa nyuklia wa Urusi katika kiwanda hicho. "Kwanza kabisa, namshukuru Rais wa Urusi kwa mwaliko wa kutembelea kinu cha nyuklia cha Kursk katika mazingira kama haya ya dharura. Sote tunajua ni kwa nini niko hapa leo pamoja na ujumbe wangu"

IAEA imeonya mara kwa mara kuhusu hatari ya kufanyika mapigano karibu na vinu vya nyuklia kufuatia uvamizi kamili wa jeshi la Urusi nchini Ukraine Februari 2022. Katika siku za mwanzo za mzozo huo, vikosi vya Urusi vilikikamata kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia kusini mwa Ukraine, na pia kikakishikilia kwa muda kiwanda kilichosimamishwa kazi cha Chernobyl katika upande wa kaskazini.

Urusi ilianzisha Agpsti 6 operesheni ndani ya mipaka ya Urusi katika mkoa wa Kursk Picha: 95th Air Assault Brigade/via REUTERS

Mapambano yamepamba moto

Ukraine ilianzisha uvamizi wa kushtukiza mkoani Kursk Agosti 6 na imesema inaendelea kupiga hatua, hata wakati vikosi vya Urusi vikiendelea kuingia ndani zaidi mashariki ya Ukraine.

Rais wa Urusi Vladmir Putin wiki iliyopita aliituhumu Ukraine kwa kujaribu kukishambulia kinu cha nishati ya nyuklia cha Kursk, ambacho kiko umbali wa chini ya kilomita 50 kutoka yanakoendelea mapigano kati ya vikosi vya Urusi na Ukraine.

IAEA ilithibitisha kuwa ilifahamishwa na maafisa wa Urusi kwamba vipande vya droni vilipatikana Alhamisi iliyopita karibu mita 100 kutoka kituo cha kuhifadhi nishati ya nyuklia cha kiwanda cha Kursk.

Ziara hiyo ya Grossi imejiri katika wakati ambapo imeripotiwa kwamba Urusi imeishambulia kwa siku ya pili mfululizo Ukraine kwa silaha nzito nzito, usiku wa kuamkia leo.

Mashambulizi ya Urusi yameua zaidi ya watu 30 Ukraine

02:10

This browser does not support the video element.

Takriban watu watano wameuwawa kufuatia mashambulizi hayo. Jeshi la Ukraine limesema kwa mara nyingine Urusi imerusha makombora ya masafa marefu ya aina mbali mbali dhidi ya miji kadhaa ya Ukraine.

Akizungumza hii leo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mashambulizi hayo pia yalijumuisha droni 81 na kuwa watu 16 walijeruhiwa.

Diplomasia yaendelea

Kuhusu juhudi za kidiplomasia, China imetoa wito kwa nchi zaidi kuidhinisha mpango wa amani kwa ajili ya Ukraine baada ya duru ya mazungumzo ya kidiplomasia na Indonesia, Brazil na Afrika Kusini ili kuunga mkono mpango wake. Li Hui ni Mjumbe Maalum wa serikali ya China kuhusu Masuala ya Ulaya na Asia. "Pande zote zina wasiwasi kuwa nchi za Magharibi zinaendelea kulegeza masharti kwa Ukraine kuishambulia mipaka ya Urusi ikitumia silaha za msaada. Kuna watu wenye nguvu katika baadhi ya nchi wanaosaidia vita hivyo, jambo ambalo linaweza kuzidisha makabiliano kwenye uwanja wa vita."

Urusi imeendeleza mashambulizi ya droni katika maeneo ya UkrainePicha: Alexander Reka/ITAR-TASS/IMAGO

China na Urusi hazikuhudhuria mkutano wa kilele wa amani uliofanyika Uswisi mwezi Juni. Urusi haikualikwa nayo China ikaamua kutohudhuria. 

Awali, Rais wa Ukraine Zelensky alisema China ilishinikizwa na nchi nyingine kutohudhuria mkutano huo wa kilele wa amani. Lakini tangu wakati huo, Ukraine inautambua mchango wa China katika mchakato wa amani, ikizingatiwa uhusiano wake wa karibu na Urusi. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine alizuru China mwezi Julai, ikiwa ni ziara ya kwanza tangu vita vilipoanza.

Marekani na NATO zinaiita China kuwa ni muwezeshaji wa Urusi katika vita hivyo. Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg kisha akasema China inatoa vifaa, na nyenzo nyingine za kielekroniki zinaoiwezesha Urusi kutengeneza makombora, silaha, mabomu na ndege wanazotumia kuishambulia Ukraine.

reuters, ap, dpa, afp,