Mkuu wa IAEA yuko Iran baada ya vikwazo kuondolewa
18 Januari 2016Katika ziara yake nchini Iran, mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Nishati ya Atomiki IAEA, anatarajiwa kufanya mazungumzo na rais wa nchi hiyo Hassan Rowhani, pamoja na mkuu wa mpango wa nyuklia wa nchi hiyo, Ali Akbar Salehi, taarifa hizo zikiwa ni kwa mujibu wa Shirika la Habari la Wanafunzi wa Iran, ISNA.
Rais Rowhani amenukuliwa na shirika hilo akisema hata baada ya kupata makubaliano kuhusu mpango wake wa nyuklia, Iran inahitaji kuendelea kuzungumza na IAEA. Rais wa Iran amesema Iran na shirika hilo wanawajibika kushirikiana kwa karibu katika ukaguzi wa hatua zilizoafikia, na kuongeza kuwa anayo imani kwamba pande hizo zitajenga msingi wa kuaminiana.
Viongozi wasifu utekelezwaji wa makubaliano
Ziara ya mkuu huyo wa IAEA Yukiya Amano inafanyika siku mbili tu baada ya shirika analoliongoza kutangaza rasmi kwamba Iran imeheshimu upande wake wa makubaliano kuhusu mpango wake wa nyuklia, hatua iliyofuatiwa na kuondolewa vikwazo dhidi ya nchi hiyo. Viongozi wa Marekani na Iran wameisifu hatua iliyofikiwa, ambayo rais Barack Obama wa Marekani amesema ni matunda ya sera yake ya maafikiano.
Obama amesema makubaliano na Iran yanadhihirisha mafanikio yanayoweza kutokana na diplomasia imara ya Marekani, na kurejelea kauli yake katika hotuba ya Umoja wa Nchi, kwamba usalama wa wamarekani utatokana na mtazamo sahihi, na wenye stahamala kwa nchi za dunia, ikiwemo Iran.
''Kama rais nimeamua kwamba Amerika yenye nguvu na kujiamini, inaweza kuhakikisha usalama kwa kuzungumza moja kwa moja na serikali ya Iran'' amesema rais Obama na kuongeza kuwa matunda tayari yameonekana. ''Katika makubaliano juu ya nyuklia ya Iran tuliyopata pamoja na washirika wetu, Iran haitapata bomu la nyuklia, na Kanda, Marekani na dunia viko salama zaidi.'' amesisitiza Obama.
Kwa upande mwingine Iran pia imeikaribisha hatua ya kuondolewa vikwazo, ambayo rais wake Hassan Rowhan ameilinganisha na ukurasa mpya katika mahusiano baina ya nchi yake na jumuiya ya kimataifa.
Tofauti nyingine zaleta vikwazo vipya
Hata hivyo rais Obama amesema bado zipo tofauti kati ya Marekani na Iran, kuhusu vitendo vya nchi hiyo alivyoviita vya ''kuyumbisha usalama''. Kama kudhihirisha tofauti hizo, Marekani imeiwekea Iran vikwazo vipya vinavyohusiana na hatua yake ya kuyafanyia majaribio makombora mapya.
Iran kupitia wizara yake ya mambo ya nchi za nje imevipinga vikwazo hivyo vipya, ikisema havina msingi wowote wa kisheria, ikizingatiwa kuwa Marekani pia inauza silaha zinazotumiwa kuwauwa wapalestina na wayemen.
Katika hatua nyingine inayoonyesha maridhiano baina ya Marekani na Iran, hapo jana nchi hizo zilibadilishana wafungwa. Tayari wamarekani watatu walioachiwa kutoka Iran wamewasili katika kituo cha jeshi la Marekani cha Ramstein Kusini mwa Ujerumani.
Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/afpe/dpae
Mhariri:Josephat Charo