Mkuu wa jeshi la Algeria jenerali Gaid Salah afariki dunia
23 Desemba 2019Alionekana kwa mara ya mwisho hadharani decemba 19, wakati wa sherehe za kuapishwa rais mpya Abdelamjid Tebboune, aliyechaguliwa wiki moja kabla katika uchaguzi ambao mwanajeshi huyo wa miaka 79 alilazimisha uitishwe licha ya upinzani wa vuguvugu la malalamiko ya umma linalopiga nchini Algeria-Hirak.
Katika sherehe hizo rais mteule Tebboune aliwapandisha cheo rais wa muda Abdelkader Bensalah na jenerali Gaid Salah na kuwapa nishani ya "Sadr"-nishati ya wastahiki ambayo kawaida hutunukiwa viongozi wa taifa.
Baada ya kumlazimisha ajiuzulu rais Bouteflika aliyekuwa amekabwa na malalamiko makubwa ya umma dhidi ya utawala wake, jenerali Gaid Salah akadhibiti jukwaa la kisiasa na kujitokeza kama kiongozi mwenye nguvu zaidi nchini Algeria mbele ya uongozi wa mpito wa kiraia ambao haukuwa ukisikika.
"Naibu waziri wa ulinzi, mkuu wa vikosi vya wanajeshi amefariki asubuhi" mtangazaji wa kituo cha tatu cha televisheni ya taifa amesema , akiisoma taarifa kutoka ikulu. Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyochapishwa pia na shirika la habari la Algeria APS, jenerali Gaid Salah amefariki baada ya kupigwa na ugonjwa wa moyo akiwa nyumbani kwake, kabla ya kupelekwa katika hospitali kuu ya kijeshi ya Ain Naadja. Jenerali Gaid Salah alijiunga na jeshi la ukombozi wa Algeria akiwa na umri wa miaka 17.
Haijulikani kifo cha jenerali Gaid Salah kitaathiri vipi shughuli za serikali mpya
Msiba wa siku tatu umetangazwa humo nchini huku jenerali Said Chengriha wa vikosi vya nchi kavu akiteuliwa kuongoza kwa muda vikosi vya jeshi la Algeria. Binafsi jenerali Chengriha aliteuliwa mwezi septemba uliopita na jenerali Gaid Salah kuongoza vikosi vya jeshi la nchi kavu.
Ni shida kuashiria kama kifo cha ghafla cha jenerali Gaid Salah kitaweza kushawishi kwa njia moja au nyengine zoezi la kukabidhiwa madaraka rais Tebboune anaesemekana alikuwa mkaribu sana wa marehemu jenerali Gaid Salah.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP