1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa jeshi Sudan kukutana na rais wa Misri leo

5 Novemba 2024

Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel-Fatah-al Burhan yuko Cairo nchini Misri alikowasili jana Jumatatu kukutana na rais wa nchi hiyo Abdel Fatah al Sisi.

Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan
Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-BurhanPicha: Dogukan Keskinkilic/Anadolu/picture alliance

Ziara hiyo ya jenerali al Burhani ni ya kwanza nchini Misri tangu nchi hiyo ilipokanusha kuhusika katika mgogoro unaoendelea Sudan.

Kwa mujibu wa msemaji wa  al Sisi,Burhani alitarajiwa kukutana kwa mazungumzo na kiongozi huyo.

Taarifa ya jeshi la Sudan ilisema rais wa Misri alimualika al Burhani kushiriki kwenye mkutano wa 12 wa jukwaa linalojadili masuala ya makaazi duniani ulioandaliwa na shirika la mpango wa makaazi la Umoja wa Mataifa-UN-Habitat.

Soma pia:Abdel Fattah al-Burhan kukutana na Rais wa Misri mjini Cairo

Ziara ya hivi karibuni kabisa ya  Burhani nchini Misri ilikuwa mwezi Februari  wakati alipokutana na al Sisi  na kujadiliana juu ya malengo ya serikali yake ya kutaka kumaliza vita na kuanzisha mchakato wa amani na uthabiti.

Ziara hii ya al Burhani imekuja wakati wanaharakati wa kutetea demokrasia wakiripoti leo Jumanne kwamba raia 10 wameuwawa katika jimbo la Al Jazira,kwenye shambulio linalodaiwa kufanywa na wanamgambo wa RSF.