1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa Kherson Ukraine aiomba Urusi kusaidia kuwaondoa raia

13 Oktoba 2022

Mkuu wa jimbo la Kherson kusini mwa Ukraine aliyewekwa na Urusi, ameiomba Urusi kusaidia kuwaondoa raia katika jimbo hilo ambalo ni kati ya manne ambayo Urusi inadai kuwa sehemu yake.

Moskau | Der Leiter der Region Cherson, Vladimir Saldo
Picha: Maksim Blinov/Sputnik/AP/picture alliance

Mwito huo umetizamwa kama ishara kuwa operesheni ya majeshi ya Ukraine kuelekea jimbo hilo kwa lengo la kulikokomboa imeshika kasi. 

Kwenye ujumbe wake kwa njia ya video, Vladimir Saldo ambaye aliwekwa na Urusi kulisimamia jimbo la Kherson, amesema wamewapendekezea raia wote wa jimbo hilo kuondoka na kukimbilia majimbo mengine.

Azimio la Baraza Kuu la UN kulaani Urusi lapita kwa kura nyingi

Hatua jhiyo ni ya kujilinda dhidi ya makombora yanayofyatuliwa. Kwenye ujumbe huo kwa utawala wa Urusi, Saldo ameomba Urusi kusaidia katika kupanga kazi hiyo.

Saldo amesema kumekuwa na ongezeko la mashambulizi ya roketi katika jimbo la Kherson na kusababisha "uharibifu mkubwa" na maafa kwa wanadamu. Kulingana na Salso, wanaoondoka watakwenda rasi ya Crimea ambayo Urusi ilichukua mwaka 2014.

Urusi yaonya dhidi ya uwezekano wa vita vya tatu vya dunia

Miji 40 ya Ukraine yashambuliwa kwa makombora ya Urusi

01:26

This browser does not support the video element.

Mwito wa Saldo umejiri siku moja tu baada ya Ukraine kusema imekomboa maeneo matano katika jimbo la Kherson.

Kherson ni miongoni mwa majimbo manne ya Ukraine ambayo Urusi ilichukua kwa njia batili.

Wakati huo huo, Urusi imeendeleza mashambulizi katika miji ya Ukraine ukiwemo karibu na mji mkuu Kiev na majimbo ya Odesa, ikitumia droni zilizotengenezwa Iran.

Hii ni siku ya nne mfululizo ambayo Urusi inafyatua makombora nchini Ukraine baada ya mlipuko ulioharibu daraja la Crimea Jumamosi iliyopita.

Mji mdogo wa Makrariv ulioko takriban kilomita 50 magharibi mwa Kiev ni miongoni mwa maeneo yaliyoshambuliwa Alhamisi na miundombinu muhimu kuharibiwa.

Ukraine yapokea mfumo wa ulinzi wa makombora wa Ujerumani

Kulingana na maafisa wa Ukraine, watu 13 wameuawa na wengine 37 wamejeruhiwa  tangu jana kufuatia mashambulizi hayo.

Kule Moscow Urusi imethibitisha kuuawa kwa askari wake watano wa akiba waliojumuishwa kikosini kufuatia wito wa Vladimir Putin mwishoni mwa mwezi uliopita. Lakini Moscow haikutoa maelezo zaidi kuhusu ni wapi waliuawa

Wiki iliyopita, waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu alisema zaidi ya askari 200,000 walijumuishwa kikosini kufuatia agiizo la Putin kushiriki kwenye uvamizi wa nchi hiyo Ukraine.

Bado kuhusu mzozo huo, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, amemtaka rais wa Urusi Vladimir kuachana na vita vyake nchini Ukraine akisema, ulimwengu hautaki kuoneka machafuko hayo yakiongezeka.

Kwenye ukurasa wake wa Twitter, Macron ameandika kuwa "Hatutaki Vita vya Ulimwengu, tunaisaidia Ukraine kujilinda nchini mwake sio kuishambulia Urusi. Rais Vladimir Putin sharti asitishe vita hivyo na aheshimu uhuru wa Ukraine,” amesema Macron na kutoa maelezo zaidi kuhusu msaada wa hivi karibuni wa nchi yake kwa Ukraine unaojumuisha zana za mashambulizi, mifumo ya ulinzi na vifaru.

Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Edogan (Kushoto) na rais wa Urusi Vladimir Putin wakikutana pembezoni mwa mkutano wa kilele wa kujenga mikakati ya Asia (CICA) mjini Astana Kazakhstan, Oktoba 13, 2022.Picha: Sputnik/Vyacheslav Prokofyev/Pool via REUTERS

Kwingineko mataifa saba tajiri zaidi ya G7, yameihakikishia Ukraine kwamba yataendelea kuipa misaada katika kipindi cha vita.

Waziri wa Fedha wa Ujerumani Christian Lindner amewaambia waandishi wa Habari mjini Washington kwamba ujenzi upya wa Ukraine utahitaji mashirika ya kimataifa ya fedha, kundi la G7, Marekani na washirika wengine kushirikiana

Kuhusu mzozo wa nishati barani Ulaya ambao umesababishwa na mgogoro wa Ukraine, Putin aliyekuwa akikutana na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan leo amependekeza Uturuki iwe kituo cha gesi ya Urusi kuuziwa nchi nyingine zikiwemo nchi za Ulaya kutumia bomba jipya la gesi.

Erdogan alimwambia Putin kwamba Uturuki inalenga kuimarisha uhusiano wake na Urusi katika sekta za nishati na usalama na kwamba inataka kurefusha makubaliano ya nafaka kati ya Urusi na Ukraine yaliyoafikiwa Julai. Muda wa makubaliano hayo unamalizika Novemba.

(AFPE,DPAE,APAE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW