1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IGAD yapendekeza kuongezwa muda wa kusimamisha vita Sudan.

27 Aprili 2023

Mkuu wa Majeshi ya Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ameashiria kukubali pendekezo la Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Afrika Mashariki (IGAD) la kuongeza muda wa kusitisha mapigano kwa saa zingine 72.

Themenpaket - Sudan
Picha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Pendekezo la Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo ya serikali za nchi za Afrika Mashariki (IGAD) la kuongeza muda wa kusitisha mapigano kwa saa zingine 72 pia linahusisha kuwapeleka wajumbe wa jeshi wa pande zote mbili zinazopingana katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, kwa ajili ya mazungumzo. Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amezungumza na mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat juu ya hali ya nchini Sudan na jinsi ya kuvimaliza vita nchini humo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken.Picha: Burhan Ozbilici/AP/picture alliance

Huku hayo yakiendelea familia za Wasudan zimekusanyika kwenye mpaka kati ya Sudan na Misri na kwenye bandari kuu, zikijaribu kuepuka vurugu zilizo nchini mwao. Familia hizo wakati mwingine zinakabiliwa na shida ya kupata chakula au malazi. Katika mji mkuu, Khartoum hali kidogo imetulia kwa siku ya pili tangu kuanza makubaliano ya kusitisha mapigano ya siku tatu. Hata hivyo milio ya risasi na milipuko ilisikika katika baadhi ya maeneo ya jiji la Khartoum hasa karibu na makao makuu ya jeshi na Ikulu yaliyoko katikati ya mji wa Khartoum. Milipuko pia imesikika kwenye kambi za jeshi zilizo karibu na eneo la Omdurman ng'ambo ya Mto Nile.

Soma:Jeshi la Sudan lasema al-Bashir anashikiliwa hospitali ya kijeshi

Wasiwasi umetanda juu ya uhakika wa mustakabali wa kudumu mapatano yoyote, hali ambayo imewafanya raia wengi wa Sudan kuchukua fursa ya utulivu uliopo japo kidogo kujiunga na maelfu ya watu wanaokimbia mapigano kati ya vikosi vya majenerali wawili wakuu wa Sudan. Mashirika mengi ya misaada yamelazimika kusimamisha shughuli zao, pigo kubwa katika nchi ambapo theluthi moja ya idadi ya watu milioni 46 wanategemea misaada.

Kushoto: Mkuu wa majeshi ya Sudan Jenerali Abdul Fattah Al Burhan. Kulia: Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo.Picha: Bandar Algaloud/Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Wasudan wanahofia pande mbili za jeshi zinazopingana zitaiendelea kupigana mara tu mazoezi ya kimataifa ya kuwaondoa raia wao yaliyoanza siku ya Jumapili yakikamilika. Kulingana na mashirika ya Umoja wa Mataifa, takriban watu 459 wameuawa na wengine zaidi ya 4,000 wamejeruhiwa.

Wakati huo huo watu kadhaa wamewasili nchiniu Saudi Arabia kwa meli za kijeshi zilizotia nanga katika bandari ya Jeddah miongoni mwao wakiwemo wanadiplomasia na maafisa wa kigeni. Watu hao wameelezea wasiwasi wao na wamesema wanawahofia wale walioachwa nyuma.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Volker Perthes amesema haoni dalili ya mapigano kumalizika hivi karibuni. Akizungumza kwa njia ya video kutoka Port Sudan Perthes, aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba pande zote mbili za jeshi hazijaonesha utayari wa kujadiliana kwa dhati.

Aliyekuwa rais wa Sudan aliyeng'olewa madarakani Omar al Bashir.Picha: Mohamed Khidir/Xinhua/Imago

Kuhusu wapi alipo aliyekuwa rais wa Sudan aliyeng'olewa madarakani Omar al Bashir hasa baada ya kushambuliwa gereza ambalo al-Bashir na maafisa wake wengi walikuwa wanazuiliwa, jeshi limejibu katika taarifa yake rasmi kwa kusema al-Bashir, Waziri wa zamani wa Ulinzi Abdel-Rahim Muhammad Hussein na maafisa wengine wa zamani walihamishiwa katika hospitali ya Aliyaa inayosimamiwa na jeshi kabla mapigano hayajaanza.

Tazama:

Nchi kadhaa zaondoa raia wake Sudan

01:21

This browser does not support the video element.

Katika hatua nyingine, mkuu wa maswala ya dharura katika Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, Dk. Mike Ryan, amewaambia waandishi wa habari kwamba ustawi wa afya kwa watu wa Sudan bado ni swala la mgogoro na kwamba mataifa yanapasa kuweka mkazo katika hilo. WHO imesema inatarajia vifo zaidi kutokea Sudan kutokana na miripuko ya magonjwa, ukosefu wa huduma muhimu pamoja na kuvurugika kwa huduma za afya,

Vyanzo:AP/RTRE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW