1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa NATO ahimiza msaada zaidi kutolewa kwa Ukraine

3 Desemba 2024

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO, wamekutana mjini Brussels katika kikao cha siku mbili leo na kesho kuzungumzia usalama na vita vya Ukraine.

Mark Rutte
Katibu Mkuu wa NATO Mark RuttePicha: Yves Herman/REUTERS

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO, wamekutana mjini Brussels katika kikao cha siku mbili leo na kesho kuzungumzia usalama na vita vya Ukraine. 

Akizungumza katika mkutano huo Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte amesema nchi wanachama wa Muungano huo zinapaswa kujadili namna ya kuipatia silaha zaidi Ukraine ili kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na uvamizi wa Urusi.

Soma zaidi. Katibu mkuu wa NATO Mark Rutte azitaka nchi wanachama kuisaidia Ukraine kwa silaha zaidi

''Ukraine inaingia katika majira mengine muhimu ya baridi na uvamizi wa Urusi hauonyeshi dalili ya kupungua. Putin anaendeleza vitendo vyake vya kikatili. Anaitumia Ukraine kama uwanja wa majaribio kwa makombora na anawapeleka wanajeshi wa Korea Kaskazini katika vita hivi haramu. Putinhana nia ya amani. Anaendelea, akijaribu kuchukua eneo zaidi kwa sababu anadhani anaweza kuvunja azimio la Ukraine na letu. Lakini anakosea. Ukraine ina haki ya kujitetea na tuna jukumu la kuwasaidia, kwa hivyo tunahitaji kuendelea kutoa msaada wetu thabiti''amesema Rutte.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ni miongoni mwa wanaohudhuria mkutano wa NATO mjini BrusselsPicha: Andreas Solaro/AFP/Getty Images

Mbali na hayo, Rutte ameongeza kuwa Ukraine inaweza pia kufanya mazungumzo ya amani na Urusi ikiwa itaamua kufanya hivyo wakati itakapokuwa na uwezo na nguvu zaidi ya kukaa katika meza moja kwa majadiliano.

Soma zaidi. Ukraine yasisitiza kukubaliwa ombi lake la kutaka kuwa mwanachama wa NATO

Mapema leo, Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken amewasili mjini Brussles na alipozungumza na waandishi wa habari baada tu ya kuwasili Blinken amesema muungano huo wa NATO lazima uhakikishe kuwa uko tayari kwa mwaka ujao wakati uchokozi wa Urusi ukiendelea dhidi ya Ukraine na vitisho vingine duniani.

Masuala muhimu ambayo yapo kwenye meza ya mkutano huo ni kuhusu ushirikiano wa kiusalama kati ya Marekani na Ulaya, vita vya Ukraine, lakini pia yapo masuala mengine kama vile kuimarisha ushirikiano miongoni mwa washirika wa NATO.

Hatua ya jeshi la Urusi kufanya mashambulizi mapya katika mji wa Dnipro wiki iliyopita ya kombora la masafa ya kati ni miongoni pia mwa ajenda ambayo itajadiliwa katika mkutano huu wa mawaziri wa mambo ya nje wa NATO.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW